Mkuu wa TAKUKURU Mkoani Manyara, Holle Joseph Makungu akizungumza na waandishi wa habari mjini Babati.
……………………………………………………………….
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoani Manyara, imefanikiwa kuokoa sh284.6 milioni, baada ya kufuatilia miradi mbalimbali ya sh7.3 bilioni, kwenye baadhi ya Halmashauri za mkoa huo.
Mkuu wa TAKUKURU mkoani Manyara, Holle Joseph Makungu aliyasema hayo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari mjini Babati.
Makungu alisema wamefanikiwa kurejesha serikalini fedha hizo katika kipindi cha utendaji kazi wao kwa muda wa miezi mitatu kwa kuanzia Januari hadi Machi mwaka huu.
Alisema wamefanikiwa kuokoa fedha hizo ambazo zimerejeshwa serikalini kupitia operesheni za uchunguzi, udhibiti, ufuatiliaji na urejeshwaji wa fedha mbalimbali kwenye baadhi ya halmashauri za mkoa huo.
Alisema katika kipindi hicho cha robo mwaka wamefanikiwa kurejesha fedha sh66.3 milioni kupitia akaunti ya Takukuru na sh180 milioni kwenye akaunti ya mamlaka ya mapato nchini (TRA).
Alitaja baadhi ya fedha hizo zilizookolewa zimetokana na operesheni tofauti ikiwemo ukwepaji kodi sh180 milioni na mrejesho wa vyama vya ushirika sh36.6 milioni.
“Fedha nyingine zilizookolewa ni sh30.2 milioni za posho za madiwani walizorejesha kwa kulipwa bila kustahili na sh16 milioni zilizorudishwa na mmoja kati ya mzabuni wa halmashauri,” alisema Makungu.
Alitaja fedha nyingine ni sh1.3 milioni za michango ya wanachama wa CCM zilizorejeshwa kwa katibu wa CCM wilaya ya Kiteto baada ya wakusanyaji wa fedha hizo kutoziwasilisha sehemu husika.
Alisema fedha nyingine ni sh400,000 zilizorejeshwa kupitia akaunti ya mkuu wa wilaya ya Kiteto kati ya sh1.2 milioni za makusanyo ya vitambulisho vya ujasiriamali.
“Huu ni utekelezaji wa maagizo na maelekezo ya Rais John Magufuli juu ya ufuatiliaji wa fedha zote za vyama vya ushirika ambapo baadhi walikopeshwa na kuendelea kukaa nazo bila kuzirejesha kinyume na utaratibu,” alisema Makungu.