Home Mchanganyiko SERIKALI KUUPATIA MUAROBAINI MGOGORO WA ENEO LA ITUHA MBEYA-WAZIRI HASUNGA

SERIKALI KUUPATIA MUAROBAINI MGOGORO WA ENEO LA ITUHA MBEYA-WAZIRI HASUNGA

0
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mhe Albert Chalamila wakikagua ramani ya eneo la Ilomba lenye mgogoro kati ya Taasisi ya Utafiti wa Kilimo-TARI Uyole na wananchi kabla ya kufanya ziara kugagua maeneo hayo wakiambatana na wananchi jana Tarehe 9 Aprili 2020. (Picha Zote Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo)
 Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mhe Albert Chalamila wakiambatana na wananchi wakikagua eneo la Ilomba lenye mgogoro kati ya Taasisi ya Utafiti wa Kilimo-TARI Uyole na wananchi jana Tarehe 9 Aprili 2020. 
Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo-TARI Uyole Dkt Tulole Bucheyeki akimuonyesha Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mhe Albert Chalamila mipaka ya eneo la Taasisi hiyo na wananchi  wa eneo la Ilomba wakati wa ukaguzi wa mashamba hayo jana Tarehe 9 Aprili 2020. 
Sehemu ya wakazi wa eneo la Ilomba wakifatilia ziara ya Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) wakati wa ukaguzi wa mipaka ya eneo lenye mgogoro kati yao na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo-TARI Uyole jana Tarehe 9 Aprili 2020. 
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mhe Albert Chalamila wakisikiliza malalamiko ya wananchi kuhusu mgogoro wa eneo la Ilomba Mkoani Mbeya jana Tarehe 9 Aprili 2020. 
…………………………………………………………………………………………………
Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Mbeya
Serikali imeanza kuchukua hatua za haraka kuumaliza mgogoro wa eneo lililo ndani ya Taasisi ya utafiti wa Kilimo (TARI UYOLE) lililopo kata ya Ilomba mkoani Mbeya.
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) jana Tarehe 9 Aprili 2020 ametangaza hatua za serikali katika kutatua mgogoro huo mara baada ya kufanya ziara ya kikazi ya siku moja mkoani Mbeya akiwa ameambatana na Kamati ya ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Mbeya iliyoongozwa na Mkuu wa Mkoa huo Mhe Albert Chalamila na kulikagua eneo hilo na kuzungumza na wananchi husika.
Waziri Hasunga ameiagiza Taasisi ya TARI Uyole kutoendelea na shughuli za utafiti mpaka hapo kesi ya mgogoro huo iliyopo mahakamani itakapotolewa uamuzi.
Kwa upande wa wananchi, Waziri Hasunga amewataka kusitisha shughuli zote za kilimo ili kusubiri maamuzi ya mahakama. Kuhusu mazao ambayo yalishalimwa na wananchi hao amesema kuwa wataruhusiwa kuvuna lakini hawataruhusiwa kuendelea na kilimo.
Wananchi hao wapatao 200 kwa mujibu wa orodha waliyoiandika na kusaini kwa ajili ya kuwasilisha malalamiko yao kwa katibu mkuu wa Wizara ya Kilimo Januari 1, 2020 wanailalamikia serikali kwa kutowalipa fidia kwa wakati hivyo kuiomba kuwalipa fidia ama kuwarudishia eneo hilo.
Eneo hilo lenye ukubwa wa Hekta 8.52 limekuwa likitumiwa na wananchi hao kwa ajili ya shughuli za kilimo pamoja na ufugaji.
Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mhe Albert Chalamila amewasihi wananchi hao kadhalika Taasisi ya Utafiti wa Kilimo TARI Uyole kuitikia maelekezo ya Waziri wa Kilimo kwani serikali itafanya maamuzi ya busara na kila mtu atapata haki yake inayostahili.
Na endapo mahakama itabaini kuwa wanastahili kurudishwa eneo hilo watapatiwa kwa mujibu wa sheria na kama itabaini hawana haki kadhalika itafanya maamuzi.