…………………………………………………………………………………..
Na.Alex Sonna,Dodoma
Mbunge wa Jimbo la Dodoma mjini,Anthony Mavunde ametoa matofali 40,000 na mifuko ya saruji 1,320 kwa kata zote ili kuboresha na kutatua kero ya miundombinu katika shule hizo.
Kauli hiyo ameitoa jana jijini Dodoma wakati akikabidhi matofali na saruji, Mavunde ambaye pia ni Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Vijana, ameweka wazi kuwa vitu hivyo vimetolewa kupitia fedha za mfuko wa jimbo.
Mavunde amesema kuwa lengo kubwa ni kusaidia ujenzi wa vyumba vya madarasa,matundu ya vyoo na nyumba za walimu na kuwataka viongozi wa kata kuhakikisha wanasimamia vyema matumizi ya vifaa hizo.
Aidha, Mavunde amesema kuwa sekta ya Elimu ni pana na kila mmoja anao wajibu wa kuungana na serikali ili kuhakikisha wanafunzi wanasoma katika mazingira mazuri ili kupata viongozi bora wa taifa.
“Ndani ya kipindi cha miaka minne hadi sasa nimetoa matofali 100,000 na mifuko 11,000 ili kutatua kero zinazoikabili sekta ya elimu, na kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia,”ameeleza Mavunde.
Kwa upande wake Afisa Takwimu wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Debora Muwinje amesema kuwa saruji na matofali hayo yametolewa kwa Shule za Msingi 38 na 2 za Sekondari.
Naye,Afisa Elimu Msingi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Joseph Mabeyo, amebainisha kuwa Halmashauri hiyo imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali kukabiliana na upungufu wa vyumba vya madarasa 1,900 kwa Shule za Msingi na Sekondari.
Kwa kuhitimisha mwaka wa fedha 2020/21 kimetengwa kiasi cha Sh.Bilioni 7 kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya shule hizo.