***********************************
NA BALTAZAR MASHAKA, Mwanza
TAWI jipya la Bilal Muslim Mission of Tanzania Kanda ya Ziwa, limeanza kazi kwa kufadhili vifaa vya huduma ya kutakasa mikono vyenye thamani ya milioni 1.5 kwa taasisi za dini na umma.
Vifaa hivyo vimetolewa jana kwa waumini wa misikiti saba iliyo chini ya Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) Mkoa wa Mwanza na Taasisi ya The Bakhiyyatullah Foundation pamoja na Wakala wa Vitambulisho vya Taifa (NIDA).
Mwenyekiti wa Bilal Kanda ya Ziwa, Alhaji Sibtaib Meghjee akikabidhi vitakasa mikono hivyo kwa Sheikhe wa Mkoa wa Mwanza, Hasani Kabeke, alisema lengo ni kusaidia jamii kupambana na virusi vya corona vinavyosababisha homa kali ya mapafu.
Alisema dunia inahangaika na watu wako kwenye taharuki kubwa, hivyo taasisi hiyo katika kuunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya tano imeamua kufadhili misikiti saba, taasisi ya Bakhiyyatullah Foundation na NIDA Wilaya ya Nyamagana kwa kuwapatia matenki hayo yatumiwe na jamii kunawa mikono.
“Tunafanya haya kwa serikali ili jamii ijue na kuonyesha uislamu ni dini ya amani tofauri na inavyotupiwa madongo.Kazi inayofanywa na Waislamu ni kwa nia njema tena bila ubaguzi,”alisema Meghjee.
Aidha aliwataka Watanzania kuchukua tahadhari na kuzuia maambukizi ya corona kwa kunawa mikono kila wakati na kuzingatia njia zinazoelekezwa na Wizara na wataalamu kujikinga na virusi hatari vya corona (Covid-19).
Kwa upande Sheikhe Kabeke, alisema vifaa hivyo ya kutakasa mikono ni muhimu katika kujikinga na corona na kuishukuru taasisi ya Bilal kwa msaada huo muhimu hasa kipindi hiki.
“Kimsingi tunashukuru Bilal kutupatia sadaka hii kwenye misikiti yetu katika vita ya kukabiliana na virusi vya corona.Wangeweza kusaidia kokote lakini wameona kheri kusaidia taasisi ya dini,” alisema.
Alieleza kuwa Meghjee amekuwa mwalimu bora katika kusaidia jamii ya watanzania maeneo mbalimbali nchini bila ubaguzi wa aina yoyote na kumwombea kwa Mungu ampe afya njema na kumwondolea watu wabaya.
Pia Sheikhe Kabeke alimshukuru Rais John Magufuli kwa kuruhusu nyumba za ibada ziendelee kutoa hufuma ya kiroho na maombi ili Mungu aliepushe taifa na janga hili hatari.
“Nitumie fursa hii kumshukuru Rais Magufuli, ni Rais pekee ambaye hakufunga nyumba za ibada na hapa watu wanamtegemea Mungu.Lakini Bilal niombe Mwenyezi Mungu akiwawezesha msiishie kwenye misikiti saba tu na pia wengine nao wajitokeze ingawa si kwamba hawawezi bali ni kiburi tu,”alisema.
Awali Sheikhe Hashimu Ramadhani wa Bilal Muslim alisema ufadhili huo umetolewa na waumini wa Shia Ithna Asheri Imamia Mwanza katika kuadhimisha siku ya Muhammad Al Mahdy aliyezaliwa miaka 155 iliyopita.