Wachimbaji wa madini ya Tanzanite wa Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, wakiwa kwenye foleni ya kuingia ndani ya ukuta unaozunguka migodi ya madini ya Tanzanite.
******************************
Na, Mwandishi wetu
Mjane wa bilionea Jubilate Ulomi, Zainabu Mkwama na watoto wake wamepewa haki kuendelea kuchimbaji madini ya tanzanite katika mgodi wa bilionea huyo na kutupwa maombi ya kusimamishwa uchimbaji.
Mdogo wa bilionea huyo,Werandumi Ulomi alikuwa amewasilisha maombi ya kutaka kusitishwa uchimbaji akidai yeye alikuwa anamiliki mgodi na marehemu kaka yake.
Afisa wa Madini mkazi katika machimbo ya Tanzanite Mirerani,Hamis Kamando alitoa maamuzi hayo jana,katika kikao baina ya wasimamizi wa mirathi ya bilionea huyo,Maafisa madini na mawakili wao,kutokana na Mgogoro wa usimamizi wa mgodi huo
Kamando alieleza taratibu za endeshaji mgodi huo zipo kisheria na leseni ya mgodi huo ilikuwa inamtambua jubilate Ulomi pekee kama mmiliki wa mgodi.
Awali katika makubaliano ya usimamizi wa mgodi huo, Werandumi ambaye pia ni mmoja wa wasimamizi wa mirathi alipewa hisa 20,Watoto watatu na mjane hisa 80.
Hata hivyo,Werandumi kupitia wakili wake,Joseph Ngilio anapinga kuanza uwekezaji kwa madai yeye na alikuwa anamiliki mgodi huo na kaka yake.
Hata hivyo,wakili wa mjane na watoto,Kennedy Mapima wanapinga hoja hiyo na kuwa tayari Mlalamikaji alisaini makubaliano juu ya uendeshaji wa mgodi huo na si kweli kama ni mmoja wa wamiliki.
Mapima alisema hakuna Mgogoro katika suala hilo ambao unaweza kusababishwa kusitishwa kuendelea kuchimbwa madini katika mgodi huo kwani kila upande una hisa.
Wakili Ngiloi alisema anapinga maamuzi ya wizara ya madini kwani uwekezaji unaoendelea unakiuka sheria na kueleza shauri hilo litafikishwa mahakamani.
Ulomi alifariki Januari 15 mwaka jana na kuacha Mali za mabilioni ambazo sasa zimeibua Mgogoro baina ya mdogo wa bilionea huyo,mjane na Watoto.
Tayari mdogo huyo wa marehemu amewafungulia kesi mjane na mtoto mkubwa wa kaka yake,akitaka waondolewe katika usimamizi wa mirathi na kubaki yeye akiwatuhumu kwa matumizi mabaya ya Mali.