Home Michezo KUSINI YAPATA KITUO CHA KISASA CHA MICHEZO

KUSINI YAPATA KITUO CHA KISASA CHA MICHEZO

0

 

****************************

Na Mwandishi Wetu
KAMPUNI ya Juvenile Sport Academy imeanza ujenzi wa kituo cha kisasa cha michezo katika Kanda ya Kusini ili kukuza vipaji vya michezo mbalimbali ukiwemo wa mpira wa miguu na riadha nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Lindi, Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Bw. Ally Kamtande, amesema kituo hicho kinajengwa katika shule ya Sekondari Nyangao iliyopo mkoani Lindi.
Amesema kwa sasa tayari wameshaanza kuboresha uwanja wa mpira wa miguu kwa kuweka nyasi bandia kwenye eneo la kuchezea huku lengo lao ifikapo Januari 2021 vijana wawe wameashaanza kutumia uwanja huo.
Bw. Kamtande amesema lengo la ujenzi huo ni kuunga mkoni juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt John Pombe Magufuli katika kukuza vipaji kwa vijana, kwani michezo ni ajira.
Amesema wameamua kujenga kituo hicho katika shule ya Sekondali ya Nyangao kwa kuwa tayari kuna miundombinu rafiki kimichezo, hivyo, hivyo amewaomba wazazi kuwaunga mkono kwa kupeleka wanafunzi pindi kituo hicho kitapofunguliwa.
Mkurugenzi huyo amesema kituo ambacho kitakuwa na walimu wa kisasa wa michezo pia kimejengwa katika mazingira bora yatakayomuwezesha kijana kujifunza kwa usahihi na furahia masomo yake.
Amesema kituo hicho kitatoa fursa kwa vijana wa mikoa ya kusini kupata eneo la kujifunzia michezo mbalimbali itakayowawezesha kuweza kujitegemea hapo baadaye na kuondokana na utegemezi. 
“Ukanda huu hauna kituo kama hiki hivyo kukamilika kwake kutakuwa mkombozi.”amesema
Kiwanja hicho pia kitaongeza idadi ya viwanja  bora vya kisasa nchini vyenye eneo zuri na la kisasa la kuchezea vikiwamo Kaitaba Mkoani Kagera, Alliance  Mwanza, JK Park Dar es Salaam.
“Niwajibu wetu wadau wa michezo kuwekeza kwenye miundombinu ya michezo na kuanzisha hizi sports academy (vituo vya michezo) ili kuinua vipaji vya watoto wetu kama ambavyo Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) ilivyosisitiza,” Mkurugenzi huyo amesema.
Kukamilika kwa kituo hicho,  kutatoa fursa kwa klabu za Ligi Kuu Tanzania Bara na ligi za chini ambazo zitahitaji kuweka kambi wakati  ligi zikiwa kwenye mapumziko kwani licha ya kuwa na mazingira mazuri na eneo zuri la kuchezea pia kutakuwa na hosteli za kisasa za kulala wachezaji pamoja na chumba cha mazoezi ya viungo.