Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe.Innocent Bashungwa akiongea na wanahabari leo baada ya kutembelea kiwanda cha kutengeneza Barakoa (Pristine Manufacturing Company Limited) kilichopo Vingunguti Jijini Dar es salaam.
Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe.Innocent Bashungwa akimsikiliza Mkurugenzi Mtendaji wa Kiwanda cha Kuzalisha Barakoa (Pristine Manufacturing Company Limited), Bw.Alnoor Lakha katika ofisi ya kiwanda hicho kilichopo Vingunguti Jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi mtendaji wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS) Dkt.Athuman Ngenya akizungumza na wanahabari baada ya kuongozana na Waziri Wa Viwanda biashara Mhe.Innocent Bashungwa kutembelea kiwanda cha kuzalisha Barakoa kwaajili ya kujilinda na Maambukizi ya Virusi vya Corona.
Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe.Innocent Bashungwa akishuhudia uzalishaji wa Barakoa ukiendelea katika kiwanda cha Pristine Manufacturing Company Limited kilichopo Vingunguti Jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe.Innocent Bashungwa akiwa katika picha ya pamoja baada ya kutembelea kiwanda cha kuzalisha Barakoa Pristine Manufacturing Company Limited kilichopo Vingunguti Jijini Dar es Salaam kujionea uzalishaji ukifanyika.
Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA), Bw.Akida Khea akizungumza na wanahabari baada ya kuongozana na Waziri Wa Viwanda biashara Mhe.Innocent Bashungwa kutembelea kiwanda cha kuzalisha Barakoa kwaajili ya kujilinda na Maambukizi ya Virusi vya Corona.
*****************************
NA EMMANUEL MBATILO
Serikali ipo makini kuhakikisha inawalinda wananchi wake dhidi ya maambukizi ya Virusi vya Corona hivyo itaendelea kushirikiana na viwanda vyote vinavyozalisha vifaa tiba kwaajili ya kujikinga na maambukizi ya virusi hivyo.
Ameyasema hayo leo Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe.Innocent Bashungwa alipotembelea kiwanda cha kuzalisha Barakoa (Face Mask) kiitwacho Pristine Manufacturing Company Limited kilichopo Vingunguti Jijini Dar es Salaam.
Akizungumza katika kiwanda hicho Mhe.Bashungwa amesema kuwa Serikali itahakikisha inatatua changamoto za upatikanaji wa malighafi kwaajili ya kutengenezea vifaa tiba kwaajili ya kujikinga na Maambukizi ya Virusi vya Corona.
Aidha Mhe.Bashungwa ameeleza kuwa atakaa na balozi wa India, Balozi wa China na kufanya kila liwezekanalo malighafi ambayo yanatoka katika nchi hizo zinakuja kwa njia ya haraka.
“Zile bidhaa zinazoingia kutoka nje ya nchi nimewaambia wafanyabiashara kwamba pale wanapokwama wawasiliane na wizara yangu tutahakikisha kama ni changamoto ambazo zipo bandarini au TRA na mahali pengine popote tunashirikiana ndani ya serikali kuhakikisha zile bidhaa ambazo hatuzizalishi zinatoka nje basi hazitacheleweshwa ili kuweza kuingia kwenye mzunguko wa usambazaji”. Amesema Mhe.Bashungwa.
Kwa upande wake Mkurugenzi mtendaji wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS) Dkt.Athuman Ngenya amesema kuwa ubora wa viwango kwa vifaa tiba hasa barakoa upo vizuri uliokidhi viwango kwaajili ya kujilinda na maambukizi ya Virusi vya Corona
“Sisi kama TBS shughuli yetu ni kuweka viwango na viwango tayari vipo na hawa ndugu wameshakuja na wameshachukua viwango na vifaa hivi (Barakoa) vimetengenezwa kulingana na viwango”. Amesema Dkt.Ngenya.
Nae Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA), Bw.Akida Khea amesema kuwa kazi kubwa ya Barakoa ni kuzuia maambukizi hivyo mwanzo wanasayansi walishauri Barakoa itumike kwa watu ambao wanamaambukizi ili wasiweze kuwaambukiza watu wengine lakini Shirika la Afya Duniani limebadili msimamo wake inasemekana kwamba kifaa kinahitajika kila mtu atumie kwani maambukizi ya Virusi vya Corona yanaambukizwa kwa njia ya hewa sio kwamba ilivyofahamika awali.
Pia Mkurugenzi Mtendaji wa Kiwanda cha Kuzalisha Barakoa (Pristine Manufacturing Company Limited), Bw.Alnoor Lakha amesema kuwa kiwanda hicho kinazalisha wastani wa barakoa kati ya elfu 20 mpaka elfu 30 kwa siku.
Pmoja na hayo Bw.Lakha amesema kuwa uhitaji wa Barakoa ni mkubwa kwasasa kulingana na hapo awali ambapo Virusi vya Corona havikuwepo.