Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akijibu hoja mbalimbali za wabunge wakati alipohitimisha hoja kuhusu Mapitio na Mwelekeo wa Kazi za Serikali na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa Mwaka 2020/2021, Bungeni jijini Dodoma, Aprili 6, 2020. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapteni Mstaafu, George Mkuchika (kushoto) baada ya Bunge kupitisha Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Taasisi zake na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2020/2021. Wa tatu Kulia ni Waziri wa Katiba na Sheria, Balozi Dkt. Augustine Mahiga, Kulia ni Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako na Wa pili kulia ni Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt Angelina Mabula. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
***************************************
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema hadi leo, hapa nchini kuna wagonjwa 24 waliothibitika kuwa na ugonjwa wa Homa Kali ya Mapafu (COVID-19) ambapo watatu kati yao, wamepona na kuruhusiwa kutoka hospitali, mmoja amefariki dunia na wagonjwa 20 wanaendelea vema na matibabu.
“Serikali imeendelea kuwafuatilia watu 685 waliokutana na wagonjwa hao ambapo watu 289 wamemaliza siku 14 za kufuatiliwa na vipimo vyao vimethibitisha kuwa hawana maambukizi ya virusi vya Corona. Watu wengine 396 waliobaki wanaendelea kufuatiliwa ili kujiridhisha iwapo hawana maambukizi ya virusi hivyo.
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Jumatatu, Aprili 6, 2019) Bungeni jijini Dodoma kwenye mkutano wa 19 wakati akihitimisha hoja ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, taasisi zake na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2020/2021.
Amesema hatua zinazochukuliwa katika kukabiliana na maambukizi ya virusi vya corona ni pamoja na kufanya ukaguzi (screening) kwa wageni wote wanaoingia nchini kutoka nje pamoja na kuwaweka katika uangalizi kwa siku 14.
“Ndege zetu tumezuia kufanya safari za nje, tumezuia wafanyakazi kwenda nje ya nchi, tumeimarisha mipaka sambamba na kuhakikisha wasafiri wote wanaoingia nchini wanalazimika kuwekwa chini ya uangalizi wa lazima kwa siku 14 kwa lengo la kudhibiti mienendo ya wasafiri chini ya ulinzi wa masaa 24,” amesema.
Waziri Mkuu amesema kutokana na umuhimu wa kuwatenga watu wanaofuatiliwa, Serikali imeagiza mikoa yote nchini itenge maeneo maalumu kwa ajili ya uangalizi na kujiridhisha iwapo hawana maambukizi.
“Hatua hii ni muhimu katika kudhibiti kuenea zaidi kwa maambukizi ya virusi vya Corona. Kayi ya hao, wengi ni wale waliotoka nje ya nchi. Maeneo hayo yametengwa kwa nia njema na yako kwa viwango tofauti kulingana na uwezo wa kifedha wa wahusika. Yako mabweni, ziko nyumba, na vyote vimewekwa kwa kuzingatia gharama mtu anayoweza kumudu,” amesisitiza.
“Tunafanya hivi ili kuondoa manung’uniko yaliyokuwepo kwamba watu wanapelekewa katika maeneo ambayo hawawezi kumudu. Na baada ya kuchukua hatua hizo, sasa hivi malalamiko hayo yamepungua.”
Akielezea hatua mbalimbali ambazo zinachukuliwa hivi sasa, Waziri Mkuu amesema Serikali inaimarisha maabara mbalimbali nchini ili ziweze kutoa huduma za upimaji ikiwemo maabara zilizopo kwenye mikoa ya Arusha, Dodoma Kigoma, Mbeya, Morogoro, Mwanza, Pwani na Tanga.
“Hospitali za Rufaa za Kanda na Mikoa nazo zinaratibiwa kutoa huduma ya upimaji sambamba na maeneo ya mipakani. Shughuli hizo za upimaji zinafanyika kwa usimamizi wa Maabara Kuu ya Taifa ya Afya ya Jamii kwa lengo la kuthibitisha ubora wa vipimo hivyo na kuratibu utoaji wa matokeo.”
“Nilishasema atakayetoa taarifa za ugonjwa ni Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, na kama itabidi nitatoa mimi mwenyewe na kama italazimika sana atatoa Makamu wa Rais au Mheshimiwa Rais mwenyewe. Hii hali ya Wakuu wa mikoa na Wilaya kutoa matamko kama alivyosema Mheshimiwa Mbunge hapa, haiku sawa.”
Waziri Mkuu amesema Tanzania imeendelea kushirikiana kwa karibu na Shirika la Afya Duniani (WHO), Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) katika kuweka mikakati ya pamoja ya kuimarisha mapambano dhidi ya Ugonjwa wa Homa Kali ya Mapafu (COVID-19) na kwamba itaendelea kufanya tathmini kuhusu changamoto zinazoweza kusababishwa na ugonjwa huo na namna ya kuzitatua.
Bunge lilikubali kupitisha sh. 312,802,520,000 kwa ajili ya Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake kwa mwaka 2020/2021. Kati ya fedha hizo, sh. 88,429,156,000 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na sh. 224,373,364,000 ni kwa ajili ya matumizi ya maendeleo.
Vilevile, Bunge liliidhinisha sh. 121,786,257,000 kwa ajili ya Mfuko wa Bunge ambapo kati ya hizo, sh. 113,567,647,000 ni za matumizi ya kawaida na sh. 8,218,610,000 ni kwa ajili ya matumizi ya maendeleo.