………………………………………………………………………………..
Na Magreth Mbinga
Tutaanza kukamata wazururaji katika jiji la Dar es salaam ambao wanatoka nyumbani asubuhi wanaenda kuzurura mjini hawafanyi kazi wanategemea wapate pesa bila kufanya kazi.
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa mkoa wa Dar es salaam Mh Paul Makonda wakati wa Uzinduzi wa Shoppers Supermarket ya Mlimani City ambapo ameonyesha kufurahishwa na uwekezaji uliofanyika na wazawa jambo lililosaidia zaidi ya Vijana 205 kupata Ajira kwa Shoppers ya Mliman City pekee.
“Njooni kwa wingi shopaz Mlimani City mjipatie bidhaa mbalimabli za Kitanzania ikiwemo vyakula na bidhaa nyingine kama za kilimo na majumbani “amesema Makonda.
Aidha RC Makonda amesema uwepo wa Supermarket hiyo licha ya kuwezesha wananchi kupata mahitaji muhimu pia serikali inapata Kodi ambapo inaelezwa kwa kipindi cha miezi nane pekee ambayo Jengo hilo kikifungwa serikali ilikosa kodi ya shilingi Bilioni 28.
Pia Mh Makonda amesema watu wanaozurura kwa kukosa kazi za kufanya endapo mtu atakamatwa kwa kosa la uzururaji atapelekwa akafanye kazi ya kuzibua mitaro na kufyeka jioni watarudi nyumbani kwao.
Hata hivyo ameendelea kuwaasa wananchi hasa wakazi wa Dar es salaam kunawa mikono mara kwa mara kwajili ya kujikinga na homa kali ya virusi vya Corona .
“Hakikisha huweki vidole puani ili kuepuka maambukizi yasiendelee na mkae umbali wa mita mbili baina ya mtu na mtu kwa kuzingatia hayo tunaweza kuishinda Corona hapa nchini kwetu”amesema Makonda.
Makonda amesema kwa mujibu wa maelezo ya Waziri wa afya Mh Ummy Mwalimu kwa siku nne mfululizo hakuna maambukizi mapya mpaka kufikia siku ya jana .
“Majengo makubwa yote kama hapa Mlimani City waweke vipima joto ili kulinda watu wanao ingia na kutoka katika maeneo hayo pia kuwe na vitakasa mikono kwaajili ya kujikinga”amesema Makonda.
Hata hivyo amemalizia kwa kusema kuwa hauwezi kukaa nyumbani kwako unasubiri ugonjwa wa Corona iishe toka ndani nenda kafanye kazi ili uweze kuendesha maisha yake na familia kwa ujumla