Home Makala Modeli Ya Tanzania kuhusu maapmbano dhidi ya maambukizi ya Corona.

Modeli Ya Tanzania kuhusu maapmbano dhidi ya maambukizi ya Corona.

0

**********************************

Maggid Mjengwa,

Dar Es Salaam.

– Kupima, Kufuatilia, Karantini
– Kuelimisha umma na kutofunga shughuli za kiuchumi
– Watafiti wameanza kuumiza vichwa kujua inakuwaje modeli hii mpaka sasa imeweza kufanya kazi

Ndugu zangu,

Viongozi wengi Afrika, kwa kuwaiga wakubwa, wamejikuta wakiingia kwenye mtego wa kuzifunga nchi zao ( Lockdown).

Kufunga nchi kwa maana ya kusimamisha shughuli za kiuchumi ni moja ya hatua za kukabiliana na kuenea kwa maambukizi ya Corona.

Hata hivyo, hatua hiyo inataka umakini mkubwa. Na kuna nchi zimeharakisha kwenda kwenye hatua hiyo na kusababisha athari zaidi kwa watu wake.

Modeli ya Tanzania bado inafanya kazi na hadi sasa imeepusha athari zaidi za kiuchumi na kijamii.

Kwanini Tanzania imefanikiwa mpaka sasa?

Nchi ina historia ya kupitia changamoto za majanga na hata vita. Yote hayo yamehitaji umma kupewa elimu na kuhamasishwa kushiriki mapambano dhidi ya majanga na hata vita.

Nchi ina historia pia ya kujiandaa na kuandaa umma kabla majanga hayajaingia. Ebola ni mfano mmoja. Maeneo ya mipakani na viwanja vya ndege Tanzania ilijipanga kwa kujenga ngome ya kujihami.

Nchi ina historia ya mfumo wa kiulinzi wa jumla- Total Defence. Kwamba kila mmoja anachukua jukumu la kuihami nchi. Kama kuna mwenye kushukiwa, kuwa na dalili za kuwa na virusi au mgonjwa na hatoi ushirikiano kwenye vyombo husika, Watanzania kwa desturi watachukua wenyewe jukumu la kumripoti mtu kama huyo.

Na mifumo yetu ya kuwa na uwakilishi wa Wajumbe wa Nyumba Kumi bado inafanya kazi kuweza kuwabaini washukiwa wanaojificha ikiwamo wageni wenye kuingia bila kupitia taratibu.

Kwa kasi ndogo ya sasa ya maambukizi, inachohitaji Tanzania baada ya kudhibiti viwanja vya ndege, ni kudhibiti mipaka ya nchi kavu na majini na huku ikiongeza nguvu kwenye elimu ya umma.

Mbali ya umma kuendelea kuhamasishwa kunawa mikono kwa sabuni na kuepuka mikusanyiko, Umma ukingwe pia na elimu na taarifa potofu ikiwamo yale yenye kuelekeza jamii kwenye kuamini abrakadabra.

Huu si wakati wa umma kulishwa ‘ matango pori’ kwa habari za tiba ya Corona kuwa ni vitunguu saumu na kujifukiza. Ni maelezo ya kienyeji sana na yenye kukiuka yale ya kitaalam kutoka kwa wataalam waliosomea na kubobea.

Na itakapofika wakati wa kulazimika kufunga nchi, kupitia elimu inayotolewa na maandalizi, umma utakuwa pia na uelewa zaidi wa hatua hizo.

Na ama hakika Corona ni janga. Watu wa dunia wanashirikiana kupambana nalo. Na kila nchi, kulingana na mazingira yake , inatafuta njia zake kwenye kupambana nalo.

Tujifunze pia kutokana na changamoto wanazopata nchi nyingi zilizochagua njia za kutaka watu wabaki majumbani na hivyo kusimamisha Shughuli za kiuchumi. Kwenye kutekeleza hayo, tumeona, kuwa jeshi na polisi pia vinatumika. Hali hii inaweza hata kupelekea uwepo wa tatizo jipya la wakimbizi wa ndani. Tumeona watu wakikimbia mijini kwenda vijijini.

Hapa kwetu, na kama nchi, njia tuliyochagua kuifuata ni sahihi kwa kuanzia. Hatujafikia hali ya kuwataka watu wetu wabaki majumbani.

Maana, amri ya Rais wetu kuwataka wageni wote kuwekwa karantini kwa siku 14, kwa gharama zao, ni sahihi. Ni kwa vile, kwetu waliobainika kuwa na virusi vya Corona bado kwa rekodi wametokea nje ya mipaka , au, kuwa na mwingiliano na waliotoka nje.

Hivyo, tusubiri sasa kuona mwelekeo wa maambukizi. Na siku 14 baada ya amri ya Rais wetu kuanza kutekelezwa, itatupa nafasi ya kuanza kuona mwelekeo wa upepo huu wa maambukizi ya Corona unavyovuma.

Na hakika, Watanzania kwa jinsi walivyo. Unapowaelimisha madhara ya jambo fulani, nao wakaelewa, basi, watatekeleza mara tatu na ulivyotarajia.

Ukweli, tangu Vita Vya Kagera, kwa tuliokuwepo, sijapata kushuhudia Watanzania wanavyoitikia wito wa mapambano kama haya ya Corona.

Hakika, haijatokea kuwaona Watanzania wakihamasika kunawa mikono kwa sabuni kama tunavyoshuhudia sasa.

Sijapata pia kushuhudia watu wenye kulalamika kuwa wananawa sana. Pale Kariakoo kwenye duka moja nilipata kumshuhudia mteja akiingia dukani na akaambiwa anawe. Akahamaki na kusema;

“ Jamani ninawe mara ngapi? Nimetoka duka la jirani nako nimenawa!” Alilalama mteja.
“ Na sisi tunataka tukuone ukinawa!” Alijibiwa. Hakukuwa na namna. Alinawa.

Kwengine nikaona ndoo nje ya duka na maandishi;
‘ Lazima Kunawa’.

Kwamba raia wameshaelewa, kuwa mengine hayana hiyari. Ni ya lazima ili kulinda afya za kila mmoja.

Njia ya kufunga shughuli na kuwataka watu kubaki majumbani ina madhara makubwa kwa uchumi wa nchi na mtu mmoja mmoja.

Afrika kwa walio wengi, kutoka kwa baba au mama nyumbani na kwenda kuhemea ndio hakika ya mlo wa jioni. Ukiwalazimisha kubaki majumbani pasipo lazima , yumkini wakitoka wataanza kusongamana kuhemea bidhaa na huduma. Hapo sasa wataambukizana zaidi.

Usimuige tembo kwa kila kitu. Walitwambia wahenga wetu. Duniani tumetofautiana. Mtu na mtu, na nchi na nchi. Wenzetu wa mataifa yaliyoendelea wana uwezo wa kuwaambia watu wao wabaki majumbani. Bado mihamala yao itasoma, kwa fedha za kutumiwa na Serikali kujikimu hata kwa wasio na kazi.Na chakula wataagizia kwa simu na kuletewa hadi mlangoni.

Afrika hakuna Serikali inayoweza kuwatumia watu wake fedha za kujikimu kwa M- Pesa, Tigo Pesa au Airtel Money. Labda Afrika Kusini!

Tofauti yetu na mataifa mengine ni kama ya Kuku wa Kisasa na Wa Kienyeji. Wa Kisasa wanaweza kuwekwa bandani na wakasuburi chakula na maji. Riziki ya kuku wa Kienyeji iko miguuni mwake.

Jaribu uwafungie kuku wa Kienyeji bandani kwa siku moja bila kuwapa punje za mtama na maji. Watatoka kwa namna wanayoijua wao.

Ukiwasogelea, kwa hasira watakuparura hata wewe mwenye kuku. Kama wasipojua, kuwa sababu za kubaki bandani ni kuwa nje kuna ugonjwa wa mdondo na kwamba hakika ya wao kupata mtama na maji ipo hata wakiwa bandani.

Hivyo, adili ya jambo hili ni kuendelea kuwa na tahadhari na kutokuwa na taharuki.
Hilo la pili laweza kuwa na madhara zaidi.