Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), Mhandisi Victor Seff akiwa kwenye kikao kazi na Waratibu wa TARURA wa Mikoa, kwenye kikao kilichofanyika katika ukumbi wa Mikutano wa TARURA Makao Makuu- Mtumba jijini Dodoma hivi karibuni.
……………………………………………………………………………………………….
Na. Erick Mwanakulya
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), Mhandisi Victor Seff amewataka Waratibu wote wa TARURA nchini kufanya ukaguzi wa mara kwa mara katika barabara na madaraja ili kubaini maeneo yanayohitaji ukarabati na kuyafanyia kazi kabla ya kuleta madhara.
Mhandisi Seff ameyasema hayo, alipokutana na Waratibu wa TARURA wa Mikoa jijini Dodoma katika ukumbi wa Mikutano wa Ofisi za TARURA Makao Makuu zilizopo Mtumba, ikiwa ni sehemu ya kikao kazi kilicholenga kutoa maelekezo na miongozo mbalimbali ya ufanyaji kazi ili kuwapatia wananchi huduma ya usafiri na usafirishaji.
Aidha, Mtendaji Mkuu amesisitiza kuwa, ukaguzi wa mara kwa mara wa miundombinu unasaidia kupunguza gharama kwani uharibifu au uchakavu wa miundombinu ukibainika mapema ukarabati wake unaweza kufanyika katika hatua za awali kwa gharama nafuu na kwamba miundombinu inapoharibika moja kwa moja gharama inakuwa kubwa sana pale inapobidi kujengwa upya.
Pia, Mhandisi Seff amesisitiza juu ya uwekwaji wa alama za barabarani hasa katika maeneo maalumu kama madaraja na maeneo yaliyoharibika ili watumiaji wa barabara watambue vizuri maeneo hayo wakati wa kupita.
‘‘Natoa maelekezo juu ya uwekwaji wa alama za barabarani kwamba, hakikisheni mnaweka alama za kudumu maana sitamsikiliza yeyote atakayekuja na sababu kuwa kibao kimeibiwa wakati angeweza kuweka kibao cha kudumu hata kwa kutumia zege maana bila kuwa na alama hizo inaweza kuwa chanzo cha ajali”, amesisitiza Mhandisi Seff.
Ili kurahisisha usimamizi wa kazi kwa mikoa yote kiongozi huyo ameeleza kuwa, anaendelea kutoa magari kwa Waratibu wote wa TARURA na kisha atatoa magari kwa Mameneja wa TARURA wa Halmashauri ili kuhakikisha wanasimamia kazi na wananchi wanasafiri kwa urahisi.
Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) unaendelea kutekeleza majukumu yake katika Mji wa Serikali Mtumba baada ya kukamilisha ujenzi wa ofisi yake na kuhamia rasmi.