******************************
Chama cha Soka barani Ulaya kimetoa onyo kwa mataifa yanayohitimisha ligi zao mapema katika kipindi hiki cha janga la Corona, na kuyatahadharisha kuwa yanaweza kupoteza nafasi zao kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa na Europa League msimu ujao.
Onyo hilo limetoka ikiwa ni siku moja baada Ubelgiji kuhitimisha ligi yake kwa kuwatangaza Club Brugge kuwa mabingwa wa msimu huu licha ya kutomalizika kwa mechi zote.
Barua ya Uefa kwenda kwa bodi na vyama vya soka katika mataifa ambayo ni wanachama wake, imeeleza kuwa kuna mpango unaotengenezwa kwa ligi zote barani humo kumalizika mwezi Julai au Agosti mwaka huu ikiwemo Ligi ya Mabingwa pamoja na Europa League ambazo ziko katika hatua ya 16 bora.
“Kwa kuwa kigezo kikubwa cha kushiriki michuano ya Uefa ni matokeo ya uwanjani baada ya ligi husika kukamilika kwa mechi zote kuchezwa, kuhitimisha ligi kabla ya wakati, kunaweza kuyafanya mataifa hayo kukosa sifa hiyo”, imeeleza barua hiyo.
Katika barua hiyo, Uefa imeeleza kuwa wana imani kuwa ligi zinaweza kurejea mwezi ujao, na mechi kuchezwa kwa masharti yatakayowekwa na mamlaka husika, na baada ya mabingwa kupatikana, ndipo msimu mpya wa ligi ya mabingwa utaanza.