Naibu Waziri anayeshughulikia maswala ya Elimu Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI), Mhe. Mwita Waitara akikagua moja ya vyumba vya madarasa yaliyojengwa katika Shule ya Msingi Manungu
iliyoko katika kata ya Sejeli wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma.
Mwonekano wa baadhi ya vyumba vitano vya madarasa ya Shule ya Msingi Manungu yaliyojengwa kwa nguvu ya wananchi wa Kata ya Sejeli wilaya ya Kongwa Mkoani Dodoma
Naibu Waziri anayeshughulikia maswala ya Elimu Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI), Mhe. Mwita Waitara akizungumza na viongozi wa Kata ya Sejeli na wilaya ya Kongwa( hawapo pichani) leo mkoani Dodoma wakati wa ziara ya kukagua vyumba vitano vya madarasa ya Shule ya Msingi Manungu.
*******************************
Na. Majid Abdulkarim KONGWA
Serikali imetoa mabati 324 kwa Shule ya Msingi Manungu iliyoko katika kata ya Sejeli, Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa Mkoani Dodoma kwa ajili ya kuezeka vyumba vya madarasa matano yaliyojengwa kwa nguvu za wananchi.
Hayo yamebainishwa na Naibu Waziri, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Mhe. Mwita Waitara leo katika ziara yake ya kikazi kukagua maendeleo ya ujenzi wa madarasa hayo katika Halmashauri hiyo.
Mhe. Waitara amesema kutokana na juhudi za wananchi katika kushirikiana na serikali katika kuleta maendeleo kwenye sekta ya elimu ndani ya wiki mbili mabati hayo ya geji 28 yatakuwa yamewasilishwa katika shule hiyo ili kukamilisha ujenzi wa vyumba vya madarasa katika shule
hiyo.
“Nataka shule zikifunguliwa baada ya janga la COVIC-19(CORONA) kuisha na wanafunzi krudi shule, madarasa hayo yaanze kutumika ili kutatua changamoto ya uhaba wa madarasa katika shule hii,”ameelekeza Mhe.Waitara.
Amewapongeza wananchi wa Kongwa na watanzania kwa ujumla kwa moyo wa kujitolea na kuhakikisha wamejenga vyumba vya madarasa katika shule hiyo,ikiwa ni kuunga mkono juhudu za Serikali katika kuboresha miundombinu ya elimu ili kutengeneza wasomi wengi watakaokuja kulitumikia taifa hapo baadae.
Wakati huohuo, Mhe. Waitara ametoa wito kwa wananchi kufuata malelekezo yanayotolewa na Serikali pamoja na wataalam wa afya kuhusu kuchukua tahadhari ili kudhibiti ungonjwa wa Covid-19(Corona) kwa kuosha mikono na maji tiririka, kutumia vitakasa mikono na taratibu nyinginezo zilizoelekezwa.
“Nitoe rai kwa wazazi na walezi wote nchini kuhakikisha wanachukua tahadhari dhidi maabukizi ya ugonjwa huo kwa watoto kwa kuwa hivi sasa wapo majumbani hivyo msianze kuwatuma kwa ndugu na minadani wakafanye shughuli nyingine kwani lengo la kutoka mashuleni ni kuchukua tahadhali ya kuepuka msongamano juu ya kukabiliana na janga la Covid- 19,” amesisitiza Mhe.Waitara.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Bw.Deo Ndejembi amesema kuwa atahakikisha anasimamia vyema mabati hayo yaliyotolewa ili vyumba hivyo vya madarasa viweze kukamilika na kutumika.