Paroko wa Parokia ya Buhingo, Padri Kelvin Enesmo Mkama akiendesha ibada ya maziko ya marehemu Simeon Hayahaya.Kushoto ni familia ya marehemu wakiongozwa na Mzee Clement Hayahaya (kushoto wa kwanza).
Katibu wa CCM Mkoa wa Mwanza, Salum Kalli (wa tatu kutoka kulia) pamoja na wenyeviti wa wilaya za Nyamagana na Katibu wa Wilaya ya Misungwi,Latifa Malimi (kulia) wakifuatilia ibada ya mazishi ya marehemu Simeon Hayahaya iliyofanyika nyumbani kwao jana.
Vijana wa Green Gurd wakiwa wamebeba jeneza la mwili wa marehemu Simeon Hayahaya (44) kuelekea kwenye makaburi ya familia kwa maziko.
Wazazi wa marehemu Simeon Hayahaya, Mzee Clement Hayahaya na mkewe wakisaidiwa kuweka shada la maua kwenye kaburi la mtoto wa jana.Picha zote na Baltazar Mashaka
***********************************
NA BALTAZAR MASHAKA, Misungwi
KATIBU wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mwanza, Salum Kalli, jana amewaongoza maelfu ya Wana CCM na wananchi wa Kijiji cha Seke,Kata ya Buhingo,wilayani Misungwi,kumzika Katibu wa Siasa na Uenezi wa wilaya hiyo, Simeon Hayahaya (44).
Mazishi ya marehemu huyo yaliyohudhuridhuwa na viongozi wa Chama na Serikali, wana CCM na wananchi wakiongozwa na Katibu wa Mkoa, yalifanyika nyumbani kwao katika makaburi ya familia.
Akitoa salamu cha Chama kwa waombolezaji, Kalli alisema kuwa jamii ina wajibu wa kushirikiana kwenye shida na raha huku ikitanguliza ubinadamu na upendo ili kutimiza dhana ya ujamaa.
“ Suala la kifo hakuna wa kukwepa sote lazima tupitie katika njia hiyo na kwa namna Mungu alivyopanga unaondokaje katika dunia hii.Tunapaswa kuachana na ukabila na vyeo tulivyo navyo kwani baada ya kifo tunaviacha.Jambo muhimu ni kudumisha upendo, mshikamano na ushirikiano tukitanguliza ubinadamu,”alisema.
Alisistiza kuwa jamii na wananchi bila kujali itikadi za vyama na dini, wakitanguliza ubinadamu na upendo miongoni mwao watajenga taifa lenye mshikamano usiotetereka na lisilo na mgawanyiko.
Aidha, aliwataka wananchi kuendela kumuomba Mungu aliepushe taifa na janga la ugonjwa wa homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona (Covid- 19) na kuepuka misongomano isiyo na sababu ambayo ni moja ya vyanzo vya maambukizi.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Misungwi Juma Sweda, alisema kuwa marehemu Hayahaya alifanya naye kazi kwa karibu na alikuwa mchapakazi, mwenye mawazo ya kujenga na maamuzi sahihi, hivyo Chama kimepata pigo kubwa.
“Kifo hakizoeleki,Simeon amepigana vita yake, imani ameilinda na mwendo kaumaliza.Tuliobaki tunalo jukumu kubwa la kujiombea ni namna gani tutajilinda na kujikinga na ugonjwa wa homa ini , ni ugonjwa hauna tiba lakini serikali imeanza kutoa chanjo na hivyo wananchi waende hospitali kupat chanjo hiyo,”alisema.
Sweda pia aliwakumbusha wananchi na waombolezaji hao kuendelea kuchukua tahadhari ya maambukizi ya virusi vya corona na kuzingatia maelekezo ya wataalamu huku wakijitahidi kukaa umbali wa mita sita kutoka mtu mmoja hadi mwingine ili kuepuka kuambukizana.
Marehemu Simeon Hayahaya alifariki Machi 31, mwaka huu, majira ya saa 12:07 alfajiri kwa ugonjwa wa homa ya ini, kabla ya mauti kumfika alitibiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Misungwi, kisha Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwanza, Sekou Toure na baadaye Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando (BMC), ameacha mjane na watoto saba, wanne wa kike na wakiume watatu.