…………………………………………………………………….
Na.Alex Sonna,Dodoma
Mchekeshaji, Emmanuel Mgaya ‘Masanja’ amepewa siku tatu kuripoti ofisini kwa Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Patrobas Katambi au kituo kikuu cha polisi kilichopo jijini Dodoma.
Agizo hilo limetolewa leo jijini Dodoma na Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Patrobas Katambi akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kuona video ya kipindi chake ambacho hurushwa na Kituo cha Televisheni cha Kimataifa cha DW, ambapo alikua akihoji wananchi wa Dodoma kuhusiana na virusi vya Covid19 ambavyo huchangia maambukizi ya ugonjwa wa Corona.
DC Katambi amesema kuwa mchekeshaji huyo alikuwa akiufanyia mzaha ugonjwa wa Corona ilihali serikali inafanya kazi kubwa ya kuhamasisha wananchi kujikinga na ugonjwa huo.
” Licha ya viongozi wetu wa Kitaifa wakiongozwa na Rais Magufuli kuwataka wananchi kufuata ushauri wa watalaamu katika kujikinga na ugonjwa huu, kumetokea utani wa kuufanyia mzaha ugonjwa huu akitaka kuthibitisha kuwa wananchi wetu hawana uelewa wowote wa Corona.
Sasa kwa mzaha huo tunataka kujua malengo yake na kwanini amefanya hivyo Dodoma wakati hata Kituo chake cha DW nchini Ujerumani wameuchukulia serious, sasa kwanini hawajafanya utani huo sehemu nyingine zaidi ya Tanzania na haswa Dodoma. Sasa nimtake afike Ofisi ya Mkuu wa Wilaya au Vituo vyetu vya Polisi ndani ya siku tatu,” Amesema DC Katambi.