********************************
Serikali imesema Mradi wa Kuboresha Elimu ya Sekondari (SEQUIP) wenye thamani ya Dola za Kimarekani milioni 500 ulioidhinishwa na Bodi ya Wakurugenzi Watendaji wa Benki ya Dunia hivi karibuni utatumika kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia katika shule za sekondari nchini.
Hayo yamesemwa jijini Dodoma na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako wakati akizungumzia mradi huo ambapo amesema pamoja na kujenga miundombinu ya shule mradi huo utatoa mafunzo kazini kwa walimu na wanafunzi kuhusu masuala ya kidijitali.
Waziri Ndalichako amesema katika kipindi cha miaka minne Serikali katika shughuli za elimu ilijikita zaidi katika kujenga miundombinu kwa sababu mwitikio wa utekelezaji wa Sera ya elimu bila malipo katika ngazi zote za elimu umekuwa mkubwa hivyo mradi huo unakwenda kuongeza miundombinu katika shule za sekondari.
“Serikali imefanya jitihada kubwa ya kuongeza miundombinu katika maeneo mbalimbali ya elimu baada ya mwitikio mzuri wa elimu bila malipo ambao utaongeza idadi kubwa ya wanafunzi wanaokwenda kujiunga na elimu ya sekondari. Mradi huu utasaidia katika kuboresha na kuongeza miundombinu katika shule za sekondari nchini ambazo zitapokea wanafunzi hao waliotokana na mwitiko wa elimu bila malipo,” amesema Profesa Ndalichako.
Ameongeza kuwa mafunzo kazini yatasaidia kuongeza ujuzi na stadi ambazo zinaendana na wakati wa sasa ili waweze kufundisha vizuri zaidi. Pia mradi huo utatoa mafunzo ya kidijitali kwa wanafunzi wa shule za sekondari.
Aidha, amesema Mradi huo utamuondolea changamoto mtoto wa kike na vikwazo ambavyo vilikuwa vinasababisha asiweze kumaliza elimu yake kwa kuhakikisha inajenga mabweni, shule maalum mpya za wasichana zenye mabweni pamoja na kuimarisha utoaji wa ushauri nasaha ili wanafunzi wanaokuwa na changamoto za kifamilia, kijamii ama mazingira ya shule wawe na mahali pa kusemea ili serikali iweze kuchukua hatua.
“Watoto wa kike wamekuwa wakipata vikwazo kutokana na umbali wa shule na kusababisha kupata changamoto wanapokwenda ama kurudi shuleni kwa hiyo kupitia mradi huu tunakwenda kujenga shule za bweni kwa ajili ya watoto wa kike,” amesisitiza Waziri Ndalichako.
Kuhusu kuondoa changamoto ya wingi wa wanafunzi darasani katika shule za sekondari iliyotokana na elimu bila malipo, Waziri Ndalichako amesema mradi huu utawezesha ujenzi wa shule katika Halmashauri mbalimbali nchini zenye wanafunzi wengi.
Aidha, Waziri Ndalichako amesema mradi huo unakwenda kunufaisha wanafunzi zaidi ya milioni sita na kuongeza kuwa serikali imefungua milango yake katika kupokea ushauri, maoni na mapendekezo kuhusu namna ya utekelezaji wa mradi huo ili kuwezesha kuwa na manufaa kwa nchi.