Mstahiki Meya wa Manispaa ya Morogoro, Mhe. Pascal
Kihanga, akiwasha Pikipiki katika hafla fupi ya makabidhiano ya Pikipiki kwa Kata zilizopo Pembezoni mwa Manispaa ya Morogoro.
Afisa Utumishi wa Manispaa ya Morogoro , Waziri Kombo,
(kushoto), akisoma taarifa fupi ya Manunuzi ya Pikipiki kwa ajili ya Kata zilizopo pembezoni wa Manispaa ya Morogoro, (kulia), Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro, Sheilla Lukuba, (katikati), Mstahiki Meya wa Manispaa ya Morogoro, Mhe. Pascal Kihanga.
*******************************
NA FARIDA SAIDY MOROGORO.
HALMASHAURI ya Manispaa ya Morogoro imenunua Pikipiki saba (7) aina ya YAMAHA zenye thamani ya Shilingi Milioni 23,100,000/= pamoja na kodi (VAT) kupitia fedha za Mradi wa uboreshaji Miji (ULGSP) katika bajeti ya mwaka wa fedha 2019/2020 kwa ajili ya kuwajengea uwezo Watumishi kwa kuboresha utendaji kazi wao.
Akizungumza na Waandishi wa Habari mara baada ya makabidhiano hayo ya Pikipiki ,Mstahiki Meya wa Manispaa ya Morogoro Pascal Kihanga, amesema Pikipiki hizo zimenunuliwa mahsusi kwa ajili ya Kata za Pembezoni ambazo Pikipiki nne (4) wamepatiwa Kata za Luhungo, Mzinga , Mkundi pamoja na Kingolwira.
Amesema Pikipiki tatu (3) zimebakia Ofisi Kuu ya Manispaa ya Morogoro kwa ajili ya kuimarisha utendaji kazi wa Halmashauri.
“Tunaipongeza sana Manispaa kwa kuwa na jicho la tatu kununua Pikipiki hizi, Kata hizi za pembezoni zinachangamoto sana haswa kwa Watendaji wake wanashindwa kuwafikia Wananchi kwa urahisi na
kushindwa kutoa huduma lakini kwa hiki walichokifanya kitatoa mwanya mzuri wa Watendaji kuwahudumia wananchi wao ipasavyo, lakini niwaombe na kumuomba Mkurugenzi wetu wa Mansipaa kwamba Pikipiki hizi zitumike katika muda wa kazi baada ya hapo wewe
mtendaji endelea na mambo yako mengine weka chombo hicho nyumbani kwani isijekuwa Manispaa imefikiria kuleta maendeleo harafu maendeleeo hayo yakageuka vifo tunajuana tabia zetu sasa tuvilinde na kuvithamini”Amesema Kihanga.
Hata hivyo amewataka Watendaji wa Kata hizo, kuvitumia vyombo hivyo vya Moto kwa malengo yaliyokusudiwa na sio kuvitumia kwa ajili ya kugeuza kuwa Bodaboda na kujipatia kipato kwa atakaye kiuka utaratibu atachukuliwa hatua za Kisheria .
Katika hatua nyingine, amewapongeza Wataalamu wa Manispaa na kuwaomba mara baada ya Miradi iliyopo kukamilika waanze kufikiria miradi mipya kwani anaamini Bajeti ijayo ya Mwaka wa fedha wa 2021/2022 Manispaa itakuwa na fedha za kutosha na kuweza kuwa na bajeti kubwa ya kihistoria.
Kwa upande wa Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro, Sheilla Lukuba, amesema Manispaa imetoa Pikipiki hizo kwa ajili ya kurahisisha huduma kwa Wananchi na kuhakikisha huduma bora zinapatikana katika Kata hizo.
Amesema kuwa matarajio yake ni kuona kuwa Pikipiki hizo zinarahisisha kwa kiasi kikubwa utekelezaji wa Shughuli mbalimbali za Serikali kwani hata maeneo yasiyofikika kwa urahisi kwa gari sasa yatafikika.
“Tuvitunze vyombo hivi, Serikali yetu ya Awamu ya Tano chini ya Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, imeonyesha moyo wa kuthamini kazi zetu nasi tuvipe heshima na kuvitumia kwa malengo tarajiwa, tusiende kuvigeuza Bodaboda na tutaweka utaratibu yule ambaye atakiuka utaratibu huu
tutamchukulia hatua kali za kisheria niwaombe Watendaji chapeni kazi tuendelee kuwahudumia Wananchi wetu katika Utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi CCM katika kufikia adhima ya Tanzania ya Viwanda na Uchumi wa Kati”Amesema Sheilla.
Aidha, Mkurugenzi amewataka Watumishi wote wa Manispaa kufanya kazi kwa bidii ili kuweza kufikia malengo na kutoa huduma bora kwa Wananchi.