*****************************
Leo tarehe 28/3/2020 Tanzania Red Cross Society (TRCS) imefanya Uhawilishaji Fedha (Cash Transfer) awamu ya kwanza kwa waathirika wa mafuriko yalitokea mwishoni mwa mwezi Januari katika vijiji vya Kipindimbi na Njinjo wilaya Kilwa mkoani Lindi.
Akimuwakilisha Rais wa TRCS Mh. David Mwakiposa Kihenzile, Mwenyekiti wa Mkoa wa Mtwara Ndg. Brighton Mkwambe amesema kwamba, TRCS imejitahidi kuhakikisha wahanga wa mkoa wa Lindi wanapatiwa msaada zaidi wa fedha kwa kuzingatia kiwango kikubwa cha madhara ukilinganisha na mikoa mingine iliyokumbwa na maafa kama hayo nchini.
Akiambatana na Kamati ya Habari na Maafa, Menejimenti na wafanyakazi wa TRCS wamewasilisha fedha hizo kwa kaya 562 kama msaada kwa wakazi wa vijiji hivyo ambapo fedha hizo zimetolewa na TRCS ili ziweze kusaidia wahanga wa mafuriko katika vijiji hivyo kukidhi mahitaji muhimu ya kibinadamu na zitaendelea kutolewa kwa mwezi Aprili na Mei.
Zoezi hilo limezinduliwa na Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Kilwa Mh. Haji Mbarouk Balozi ambapo ameishukuru TRCS kwa msaada waliondeendelea kutoa kwa jamii ya vijiji hivyo na kuahidi kuunga mkono jitihada zinazofanywa na TRCS katika kuisadia jamii.
Aidha, Mwenyekiti wa Kamati ya Maafa Wilaya ya Kilwa Ndg.Renatus B. Mchau amepongeza juhudi za TRCS katika kurudisha hali ya maisha ya jamii kama ilivyokuwa kabla ya maafa hayo na amewataka wanufaika wa msaada huo kutumia fedha walizopata kwa usahihi kama ilivyokusudiwa.
Zoezi hilo la Uhawilishaji wa Fedha limekwenda sambamba na utoaji wa elimu juu ya Ugonjwa wa Virusi vya Corona kwa wanufaika wa msaada huu na baadhi ya voluntia wa mkoa wa Lindi kama ilovyoelekezwa na Wizara ya Afya.