********************************
Kuanzia tarehe 19.03.2020 hadi 26.03.2020 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi ULRICH O. MATEI alifanya ukaguzi wa kutembelea Mahabusu na Wafungwa katika Magereza ya Ruanda, Kyela, Tukuyu na Mbarali akiwa ameongozana na mwakilishi toka Ofisi ya Mwendesha Mashitaka
wa Serikali Mkoa wa Mbeya ndugu BASILIUS NAMKAMBE, Kaimu Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Mbeya ASP BONIPHACE V. LUAMBANO, Wakuu wa Upelelezi wa Wilaya za Mbeya, Chunya, Mbalizi, Mbarali, Kyela na Rungwe na
“Liaison Officers” wa Wilaya hizo.
Lengo la ziara hiyo ilikuwa ni kuangalia mlundikano wa Mahabusu katika Magereza Mkoa wa Mbeya pamoja na kusikiliza kero zao, changamoto walizonazo kuhusu Jeshi
la Polisi ili kuona mienendo mizima ya kesi zao na kuona namna ya kutatua changamoto hizo kwa kushirikiana na vyombo vingine vya haki jinai kama vile Magereza, Mahakama na Ofisi ya Mwendesha Mashitaka wa Serikali.
Jumla ya Mahabusu na Wafungwa aliowakuta katika Magereza hayo ni 1424, kati yao Wafungwa ni 770 na Mahabusu walikuwa 654 wenye kesi za Mauaji, Uhujumu
Uchumi, Ugaidi Unyang’anyi wa kutumia silaha na kesi ndogo ndogo. Jumla ya Mahabusu wanaosubiri kikao cha Mahakama Kuu baada ya Committal Proceedings ni
196, jumla ya Mahabusu wanaosubiri kibali kutoka kwa Mkurugenzi wa Mashitaka nchini ni 22, Mahabusu ambao majalada yao yapo ofisi ya Mwendesha Mashitaka wa
Serikali wakisubiri maamuzi ni 50 na Mahabusu ambao upelelezi bado haujakamilika ni 68 hii ni kutokana na baadhi ya kesi zinasubiri majibu ya sampuli [DNA]
zilizopelekwa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali, nyingine zinasubiri majibu kutoka Kitengo cha Uchunguzi wa Kisayansi [FORENSIC BUREAU UNIT].
Aidha katika kuhakikisha msongamano wa Mahabusu unapungua katika magereza, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya SACP ULRICH MATEI alimshauri Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Mwendesha Mashitaka wa Serikali Mkoa wa Mbeya BASILIUS NAMKAMBE kuwafutia mashitaka Mahabusu wenye makosa madogo madogo [Petty Offences] na ndipo Mwakilishi huyo wa Mkurugenzi wa Mwendesha Mashitaka nchini [DPP] aliwaondolewa mashitaka [Nolle Prosequi] Mahabusu saba [07] wa makosa ya uzembe na ukorofi, shambulio na wizi kati yao wanaume watano [05] na wanawake wawili [02] kwa mujibu wa kifungu 91 (1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai sura ya 20 kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2002 [CAP 20 – RE – 2002].
Ziara hii imekuja kutokana na maelekezo kutoka kwa Inspekta Jenerali wa Polisi SIMON N. SIRRO kuhakikisha msongamano wa Mahabusu katika Magereza na vituo vya Polisi unapungua, hivyo Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limejiwekea mpango mkakati wa kuhakikisha hadi kufikia April 15, 2020 kesi zote 68 ambazo upelelezi wake haujakamilika zinakamilishwa.
KUKAMATWA KWA MTUHUMIWA WA KUJIPATIA MALI KWA NJIA YA UDANGANYIFU.
Jeshi la Polisi mkoani Mbeya linamshikilia ADELHARD METHOD @ MGENI [37] Mfanyabiashara na Mkazi wa Njombe kwa tuhuma za kujipatia mali kwa njia ya
udanganifu kwa kutoa hundi hewa ya malipo. Mtuhumiwa alikamatwa mnamo tarehe 24/03/2020 majira ya saa 12:00 mchana huko mkoani Morogoro akiwa kwenye harakati za kutoroka baada ya kufanya matukio kadhaa maeneo mbalimbali.
Mbinu anayotumia mtuhumiwa ni kwenda kwenye maduka makubwa ya wafanyabiashara wanaouza bidhaa mbalimbali na kufanya mazungumzo nao kama mteja anayehitaji kununua bidhaa za jumla na kisha kuchukua namba za simu za wafanyabiashara hao na baada ya siku mbili hadi tatu upiga simu kwa kutumia laini zilizosajiliwa kwa njia za udanganyifu kwa wafanyabiashara hao kwa lengo la kuagiza mzigo na hufanya ushawishi kwa wafanyabiashara hao kwa kuomba afanya malipo kwa njia ya hundi na pindi atakapotumiwa namba ya akaunti uandaa hundi hewa na kisha kuituma kwa mfanyabiashara husika kwa njia ya Whatsapp.
Baada ya mwenye duka kuthibitisha kupata nakala ya hundi hiyo, mtuhumiwa atatuma Gari kwenda dukani kuchukua mzigo na kisha kutoweka. Mtuhumiwa
amekiri kuwa uwa anatengeneza hundi hewa ambayo namba ya akaunti iliyopo kwenye hundi hiyo uwa imefungwa [Closed Account], Domant au haina fedha.
Ni kwamba mtuhumiwa utengeneza hundi hewa ambayo namba ya akaunti iliyopo kwenye hundi hiyo uwa imefungwa [Closed Account], Domant Account au uwa haina fedha ndani yake na mara baada ya kuchukua mzigo mhusika akienda kuangalia kwenye akaunti yake hatakuta ongezeko lolote la fedha.
Mtuhumiwa amekiri kufanya uhalifu mikoa ya Mbeya, Songwe – Tunduma na Dodoma na mnamo tarehe 12/03/2020 alifanya udanganyifu na kuiba mali yenye
thamani ya Tshs.9,660,000/= kwenye duka la BENEDICTO MBILINYI [55] Mfanyabiashara na Mkazi wa Block “T” Jijini Mbeya.
Mtuhumiwa anahusishwa na matukio mbalimbali ya Kughushi, Wizi wa kuaminiwa, Wizi na udanganyifu kwa
kutumia hundi hewa, Mtuhumiwa atafikishwa mahakamani mara baada ya upelelezi wa mashauri haya kukamilika.
KUINGIZA GARI NCHINI BILA KULIPIA USHURU.
Jeshi la Polisi mkoani Mbeya linawashikilia watuhumiwa wawili BAKARI WALII SEMVUA [31] Mfanyabiashara na mkazi wa Mbagala Jijini Dar -es- Salaam na VICTOR JIMMY BROWN [25] Dereva/fundi, mkazi wa Tabata Segerea Jijini Dar – es- Salaam kwa tuhuma za kuingiza Gari nchini bila kibali.
Watuhumiwa walikamatwa katika misako na operesheni mbalimbali zinazoendelea huko eneo la Mafiati, Kata ya Manga, Tarafa ya Sisimba, Jiji la Mbeya katika barabara ya Mbeya – Iringa baada ya Jeshi la Polisi kuweka mtego na kufanikiwa kuwakamata watuhumiwa wakiwa na Gari hilo lenye namba za usajili T.515 DNK aina ya BMW rangi ya blue na Chassis Namba.WBA 52030CK64536 kutoka nchini
Zambia wakiwa wanaelekea Dar es Salaam.
Baada ya kuikamata gari na watuhumiwa walifanyiwa mahojiano kwa kuwashirikisha Maafisa wa Mamlaka ya Mapato Tawi la Mbeya [TRA] upande wa ushuru na forodha
na kubaini kuwa Gari hiyo iliingizwa nchini kama IT na kusafirishwa kupelekwa Tunduma kwa lengo la kupelekwa nchini Zambia ambapo ilifikishwa mpakani Tunduma tarehe 07/03/2020 ikiendeshwa na mtuhumiwa BAKARI WALII SEMVUA lakini ilipofika tarehe 17/03/2020 dereva huyo akiwa na VICTOR JIMMY BROWN waliamua kuondoka/kuiba Gari hiyo huku wakiwa wameweka
“plate” namba T.515 DNK ambayo siyo ya Gari hilo. Upelelezi unaendelea.