Eneo la kanisa la Anglikana lililopo Mtoni-Buza katika Manispaa ya Temeke jijini Dar es salaam
Eneo la kanisa la Anglikana lililopo Mtoni-Buza katika Manispaa ya Temeke jijini Dar es salaam
Mkuu wa Kitengo cha Kodi kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Bw. Denis Masami (wa pili kulia) akimuhoji mmoja wa raia wa Kichina (ambaye hakuwa tayari kutaja jina lake) anayemiliki kiwanda ndani ya eneo la kanisa la Anglikana lililopo Mtoni-Buza katika Manispaa ya Temeke jijini Dar es salaam wakati maafisa wa kodi walipotembelea eneo hilo lenye jumla ya ekari 410 na halijalipiwa kodi tangu mwaka 2005.
***********************************
Na. Hassan Mabuye, Wizara ya Ardhi
Eneo la kanisa la Anglikana lililopo Mtoni-Buza katika Manispaa ya Temeke jijini Dar es salaam limetumika kukwepa kodi ya pango la ardhi kwa kuendesha biashara vikiwemo viwanda vya wachina na maduka makubwa.
Hayo yamebainika baada ya Mkuu wa kitengo cha Kodi kutoka Wizara ya Ardhi Bw. Denis Masami kutembelea eneo hilo lenye jumla ya ekari 410 ambalo limemilikishwa kwa matumizi ya makazi na siyo biashara.
Mkuu wa kitengo cha kodi alilazimika kufika katika eneo la taasisi hiyo baada ya kukaidi kulipa kodi ya pango la ardhi kwa muda mrefu kuanzia mwaka 2005 hadi sasa ambapo maafisa ardhi kutoka Manispaa ya Temeke wamekuwa wakipeleka hati za madai mara nyingi bila ushirikiano wowote kutoka kwa Taasisi hiyo.
Aidha kwa mujibu wa mkuu huyo taasisi hiyo imebadili matumizi ya uendelezaji katika eneo hilo na wameweka wapangaji wanafanya biashara mbalimbali.
Baadhi ya maeneo wameweka wapangaji na wamejenga kituo cha mafuta, maduka zaidi ya 200 na yote yanafanya biashara, garage na viwanda vinavyozalisha bidhaa mbalimbali.
Hata hivyo kutokana na shughuli zote hizi za kibiashara zinazofanywa katika eneo hili la kanisa, ni wajibu wao kulipa kodi ya pango la ardhi kwa kuwa linatumika kibiashara tofauti na taratibu za umilikishaji ambazo zilihusu eneo la ibada kitu ambacho sio cha kweli.
Ikumbukwe kwamba tahere 27 Januari 2019 Waziri wa Ardhi, Nyumba na maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi alifuta kodi ya pango la ardhi kwa taasisi za dini na taasisi nyingine zinazotoa huduma, japo kuwa agizo hili halihusu taasisi zinazofanya biashara na kupata faida.