******************************
Na Magreth Mbinga
Tufuate maagizo kutoka Serikali Kuu na tuzingatie maelekezo ya wataalamu wa afya ili tuweze kupambana na janga hili la Corona.
Ameyasema hayo leo Meneja wa Soko la Samaki Feri Jijini Dar es Salaam Bw.Denis Mlema baada ya kutembelewa na mwandishi wetu na kuelezea namna wafanyabiashara wa soko hilo wanavyojikinga dhidi ya maambukizi ya Virusi vya Corona.
Akizungumza ofisini kwake Bw.Mlema amesema wanao maafisa afya ambao wanatoa elimu kila siku kuhusu kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni.
“Tunapokea watu elfu nane hadi elfu kumi kwa siku tunalazimika kutoa elimu kila siku kuhusu kujikinga na ugonjwa wa Corona”amesema Bw.Mlema.
Pia afisa afya wa soko hilo Bw.Harold Matee amesema wanawalazimisha wafanyabiashara kunawa mikono kwa wale ambao wanakaidi wanawazuia kuingia sokoni hapo.
“Tunatoa elimu kwa wafanyabiashara wanapo kohoa watumie kiwiko kujizuia na wakati wa mnada wakae mbalimbali ili kujikinga zaidi na virusi hivyo”amesema Bw.Matee .
Vilevile amewataka wafanyabiashara wasalimiane kwa kupungiana mikono waache kushikana au kukumbatiana kama walivojizoesha na wameweka vitendea kazi kila mlango wa kuingilia sokoni hapo.
Sanjari na hayo afisa mazingira wa soko hilo ndugu Mary Mkwavi amesema wanahakikisha soko linakuwa safi wakati wote pia tahadhari zinachukuliwa na matangazo yanawekwa kila kona ili kuwakumbusha watu wazingatie usafi.
Hata hivyo Mkwavi amemalizia kwa kusema kuwa wanahakikisha soko lao linakuwa safi muda wote uchafu unakusanywa na kuwekwa sehemu husika na amewataka wafanyabiashara wa soko hilo wachukue tahadhari na ugonjwa huo wa Corona.