****************************
NA EMMANUEL MBATILO
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imekutana na viongozi wa vyama vya siasa kwa lengo la kuzungumzia masuala ya maandalizi ya uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika baadaye mwaka huu.
Akizungumza katika Mkutano huo, Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) nchini Tanzania, Jaji Semistocles Kaijage amesema kuwa uboreshaji wa awamu hii kama ulivyokuwa ule wa mara ya kwanza utawahusu wapiga kura wapya ambao ni raia wa watanzania waliotimiza miaka 18 au watatimiza umri huo siku ya Uchaguzi Mkuu, zoezi hili pia litawahusu wale wanaoboresha taarifa zao mafalani walihama kutoka maeneo yao ya awali na kuhamia maeneo mengine yakiuchaguzi na wale ambao kadi zao zimeharibika au kupotea.
Aidha amesema kuwa zoezi hilo pia litawahusisha kuwaondoa kwenye daftari wapiga kura waliofariki na wengine waliopoteza sifa kwa mujibu wa sheria
Hata hivyo Jaji Kaijage amesema kuwa kimsingi awamu hii ya pili ya uboreshaji itawahusu wapiga kura ambao hawakupata fursa kujiandikisha katika awamu ya kwanza
“Uboreshaji wa daftari awamu ya pili ambao utaenda sambamba na uwekaji daftari la awali utafanyika katika ruti tatu, ruti ya kwanza inatarajiwa kuanza tarehe 17 mwezi Aprili mwaka huu”. Amesema Jaji Kaijage.
Pamoja na hayo Jaji Kaijage amesema Katika uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura la awamu ya pili vituo vinatarajiwa kufunguliwa saa 2 asubuhi na kufungwa saa 12 jioni kwa muda wa siku nne mfululizo.