*****************************
NA EMMANUEL MBATILO
Serikali kupitia Wizara ya Viwanda na Biashara imewaelekeza Shirika la Viwango Tanzania (TBS),kushirikiana kwa karibu na wazalishaji waliopo na wengine wapya wanaonesha nia ya kuzalisha bidhaa ya Vitakatisha Mikono kuona ni namna wananvyoweza kuongeza upatikanaji wa bidhaa hiyo sokoni.
Wizara kwa kushirikiana na taasisi zake za usimamizi wa soko,itaendelea kufanya ukaguzi na uchunguzi sokoni ili kubaini endapo kuna vitendo vyovyote vya udanganyifu au vinavyokiuka sheria zinazosimamiwa na taasisi hizo katika kuingiza, Kuzalisha,kusambaza na kuuza bidhaa hizo.
Ameyasema hayo leo Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe.Innocent Bashungwa Jijini Dar es Salaam baada ya kukaa kikao na wadau mbalimbali wa viwanda na biashara kuona ni namna gani wanaweza kutatua changamoto ya ukosefu wa vifaa vya kujikinga na maambukizi ya virusi vya Corona hapa nchini.
Akizungumza katika Mkutano huo Mhe.Bashungwa amesema kuwa kupitia wizara yake pamoja na taasisi zilizopo kwenye wizara hiyo watahakikisha wafanyabiashara hawajishughulishi na vitendo vya kuficha bidhaa,kuongeza bei kiholela, kuzalisha na kuuza bidhaa zisizokidhi viwango vya ubora vya kitaifa na matendo mengine kama hayo ambayo yanamuathiri mlaji.
“Nawaelekeza TBS na FCC kuendelea kuchunguza uzalishaji na uingizaji wa bidhaa unaozingatia viwango vya ubora na ushindani wa soko ili bidhaa hizi za kujikinga na maambukizi ya virusi vya Corona zipatikane kwa urahisi, zikidhi matarajio ya matumizi na zipatikane na kwa bei ya soko:.Amesema Mhe.Bashungwa.
Pamoja hayo Mhe.Bashungwa amesema Wizara yake itandelea kuunga mkono juhudi za wawekezaji katika kutoa mchango kupitia kazi zao kwa jamii katika nyakati za dharura ili kuhakikisha kuwa watanzania wananufaika na kustawi kutokana na uwepo wa uwekezaji wao.
Nae Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS),Dkt. Athuman Ngenya ameeleza kuwa shirika hilo limebainisha umuhimu wa wazalishaji wa bidhaa za kujikinga na maambukizi ya Virusi vya Corona hususani kwa wazalishaji wa vitakasa mikono (Hand Sanitizers) kuzingatia viwango vilivyowekwa kitaifa na shirika hilo katika uzalishaji wa bidhaa husika.
“Kiwango kilichowekwa kwa uzalishaji wa vitakasa mikono ni NaTZS 1650:2014.Kiwango hiki kinahusisha pia uwepo wa kileo (alcohol) ya walau asilimia 60 kuwezesha vitakasa mikono kuweza kufanya kazi iliyokusudiwa”. Dkt.Ngenya.
Hata hivyo Dkt.Ngenya ameongeza kuwa bidhaa zote zinazoingia wanahakikisha zinakuwa na ubora wa viwango ili visiweze kumsumbua mtumiaji.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Manunuzi MSD, Bw.Abdul Mwanja amesema kuwa mahitaji ya vifaa tiba kwaajili ya kujikinga na maambukizi ya Virusi vya Corona ni takribani shilingi 350,000 ambapo mpaka sasa bei ya vitakatisha mikono lita ni Lita 5 shilingi 85,000, robo lita shilingi 5,500.