Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani,(kushoto) Naibu Waziri wa Nishati Subira Mgalu,(kulia) wakiwa kwenye kikao na Wakandarasi wanaotekeleza mradi wa Peri Urban,Mkoani Dodoma, Machi 19,2020.
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani na Katibu Mkuu, Mhandisi Zena Said,(kushoto) wakiwa kwenye kikao na Wakandarasi wanaotekeleza mradi wa Peri Urban,Mkoani Dodoma, Machi 19,2020.
****************************
Hafsa Omar-Dodoma
Wakandarasi wanaotekeleza mradi wa umeme pembezoni mwa miji ( Peri-Uban) wametakiwa kukamilisha kazi ya usambazaji umeme katika maeneo waliyopangiwa ifikapo Juni, 2020 la sivyo watachukuliwa hatua za kisheria.
Maagizo hayo yametolewa na Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani, Machi 19, 2020, mkoani Dodoma wakati wa kikao chake na Wakandarasi wanaotekeleza mradi huo.
Kikao hicho kilihudhuriwa na Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Zena Said, Kaimu Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu Mhandisi Edward Ishengoma, Kamishna Msaidizi wa Umeme, Mhandisi Innocent Luoga pamoja na viongozi mbalimbali wa Wizara, Taasisi.
Dkt. Kalemani aliwaelekeza wakandarasi wa mradi huo kuweka mpango madhubuti ambao utabainisha vijiji vyote ambavyo havijawekewa umeme na mpango huo uoneshe ni lini vijiji hivyo vitapelekewa umeme ndani ya muda uliopangwa.
Aidha, aliwataka wakandarasi hao kufanya kazi kwa bidii ili kuhakikisha ndani ya muda waliokubaliana wawe tayari wameanza kuwasha umeme kwenye vijiji na miezi miwili inayofuata waitumie kusambazia wananchi umeme majumbani.
Aidha, aliwaagiza wakandarasi wote wa mradi huo kupeleka orodha ya vijiji vinavyosambaziwa umeme kwa Wakuu wa Mikoa, Wilaya, wenyeviti wa vijiji na mtaa ili viongozi hao wasaidie katika ufuatiliaji wa mradi huo.
Pia, aliwataka kuhakikisha kuwa nguzo zote ambazo zimelazwa chini kwenye maeneo yao, ziwe zimesimikwa na nguzo ambazo zimesimikwa bila kuwa na nyaya, ziwe zimefungwa nyaya ndani wa mwezi huu.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu aliwataka wakandarasi hao kuupa kipaumbele mradi huo muhimu katika nchi na kwamba wanachotaka kuona kwasasa ni uwashwaji wa umeme katika maeneo hayo.
Alisema, ana imani kuwa, wakandarasi hao watafuata maelekezo aliyoyatoa Waziri wa Nishati na kuyafanyia kazi.
Naye, Katibu Mkuu, Mhandisi Zena Said, aliwakumbusha wakandarasi hao kuwa, Serikali imewapa fursa na kuwaamini hivyo na wao wanatakiwa kutoiangusha Serikali kwa kumaliza kazi zao kwa muda uliopangwa.
Vilevile, aliwataka wasimamizi wa miradi hiyo ya umeme kufanya kazi kwa weledi na kuwasimamia ipasavyo wakandarasi hao ili kuhakikisha wanamaliza kazi zao kwa mujibu wa mkataba.