Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Profesa Shukrani Manya akisafisha mikono kwa kutumia kitakasa mikono Makao Makuu ya Tume ya Madini jijini Dodoma tarehe 20
Machi, 2020.
******************************
Na Greyson Mwase, Dodoma
Machi 20, 2020
Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Profesa Shukrani Manya amesema kuwa Tume ya Madini Makao Makuu pamoja na Ofisi zilizopo chini yake zimejipanga katika kukabiliana na maambukizi ya virusi vya korona.
Akizungumza jijini Dodoma leo tarehe 20 Machi, 2020 amesema kuwa hatua hiyo ni sehemu utekelezaji wa wito wa Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Dkt. John
Pombe Magufuli, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu na Miongozo ya Shirika la Afya Duniani (WHO) wa kuchukua hatua mbalimbali za tahadhari ili kujikinga na maambukizi ya virusi vya COVID 19 vinavyosababisha homa ya korona.
Alisema tayari Ofisi ya Tume ya Madini imeweka vitakasa mikono pamoja na maji tiririka kwenye ofisi zake lengo likiwa ni kuwakinga watumishi wake na wadau wa madini
wanaotembelea ofisi hizo kwa ajili ya kupata huduma mbalimbali na maambukizi ya korona.
Aliongeza kuwa, Ofisi za Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa zimeweka vitakasa mikono na maji tiririka na kuwataka wadau wa madini wanaotembelea ofisi hizo kuanza kuvitumia ili kujikinga na maambukizi hayo.
Alisema hatua zilizochukuliwa na Tume Makao Makuu na Ofisi za Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa katika kuzuia kusambaa kwa virusi vya COVID 19 vinavyosababisha homa ya Korona ni pamoja na kuepuka msongamano, kunawa mikono vizuri kwa maji safi titirika na sabuni, au maji yenye dawa, kutumia vitakasa mikono, kutumia vikinga pua na mdomo (masks), kuepuka kugusana, kukaa mbali na mtu mwenye dalili za mafua na mwenye historia ya kusafiri katika nchi zenye mlipuko wa ugonjwa huo.
Katika hatua nyingine Profesa Manya aliwataka wachimbaji wa madini kuepuka mikutano isiyo ya lazima na kuepuka misongamano ikiwa ni pamoja na kufuata
maelekezo mengine yanayotolewa na Serikali.
“Ikumbukwe kuwa hadi sasa hakuna tiba au chanjo dhidi ya virusi vya korona lakini kwa sababu virusi hivyo vinaleta dalili mfano wa zile za mafua makali, mchanganyiko wa tiba unatumika kupunguza athari za virusi vya korona, hivyo wachimbaji wa madini wanatakiwa kuchukua tahadhari kubwa kwenye shughuli zao cha utafutaji na uchimbaji wa madini.” alisema Profesa Manya.
Aidha katika hatua nyingine, Profesa Manya amewataka Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa kuhakikisha wanapunguza msongamano wa watu pamoja na kuweka maji tiririka na vitakasa mikono kwenye masoko yote ya madini na vituo vya ununuzi wa madini nchini.