*************************
Na Magreth Mbinga
Chama cha wananchi CUF kinatoa pongezi kwa juhudi ambazo Serikali imechukua katika kupambana na maambukizi ya virusi vya Corona ikiwa ni pamoja na kutangaza mara kwa mara njia za kudhibiti na hatua za dharura za kuchukua pindi dalili zinapodhihirika.
Amezungumza hayo mwenyekiti wa chama hiko Prof Ibrahim Lipumba kwenye mkutano wake na waandishi wa habari ofisini kwao buguruni jijini Dar es salaam na kusema kuwa Serikali imetoa amri ya kufunga shule na vyuo ili kupunguza mazingira ya mikusanyiko.
Pia amesema kwakuzingatia tahadhari dhidi ya maambukizi ya virusi vya Corona na ushauri wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na agizo la Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chama kimeamua kusitisha ziara zote za mwenyekiti wa chama Taifa kwa mwezi mmoja.
“Baraza kuu la Uongozi la Taifa liliishauri Serikali kuongeza uwezo wa kupima maradhi ya COVID 19 hasa katika viwanja vya ndege vya kimataifa ,hospitali na vituo vya afya kuweka taratibu za karantini,wadi za kulaza na katibu wagonjwa ikiwa ugonjwa utaibuka”amesema Prof Lipumba.
Prof Lipumba amesema Serikali kwa kushirikiana na Jumuiya ya Kimataifa hasa WHO iandae mkakati madhubuti wa kukabiliana na mlipuko wa COVID 19.
Vilevile amesema kama nchi watumie kadhia ya virusi vya Corona kama fursa ya kujenga mfumo imara wa huduma za afya za msingi na amesisitiza kinga ya maradhi ni kuishi katika mazingira safi.
Sanjari na hayo amesema Chama Cha wananchi CUF kinato wito kwa Vingozi wa Dini kuongeza Dua na maombi ili Mungu awape nafuu kwakuzingatia hali ya maisha ya Watanzania walio wengi ni rahisi sana ugonjwa huu kuenea kwa kasi kupitia vyombo vya usafiri.
“Tunatoa wito kwa wananchi wote kuzingatia maelekezo ya kitaalam ya kujikinga na maambukizi ya maradhi haya”amesema Prof Lipumba.