********************************
Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Mhe. Daniel Chongolo, amewaagiza wata alaamu wa Afya Wilayani hapo kuanza mara moja kutoa elimu ya kujikinga na virusi vya Corona kwenye nyumba za Ibada ikiwemo Makanisani na Misikitini.
Aidha Mhe. Chongolo ameagiza pia elimu hiyo kutolewa kwenye vituo vya daladala ili kuwasaidia wananchi kutambua namna ya kutumia na kujikinga na Virusi hivyo.
Mhe. Chongolo ametoa agizo hilo leo katika kikao cha zarura kilichofanyika katika ukumbi wa Afya ambapo kimehusisha Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Idara ya Afya, watendaji pamoja na viongozi wa Dini .
Amesema kuwa lengo la kikao hicho cha zarura ilikuwa ni kujadili namna na hatua zitakazo chukuliwa katika kudhibiti virusi hivyo ili visiweze kusambaa pamoja na kutoa elimu ya kutosha kwa watumishi sambamba wananchi katika Wilaya hiyo.
Amesema kutokana na kuingia kwa Virusi hivyo vya Corona katika jiji la Dar es Salaam, wataalamu hao wa Afya wa Wilaya hiyo wanapaswa kutoa elimu madhubuti kwenye maeneo ambayo ni lazima wananchi kuyatumia kama vile Vituo vya daladala ikiwemo vya mwendokasi, nyumba zaibada kuhusu namna ya kujikinga na virusi hivyo.
Amefafanua kuwa katika elimu hiyo pia itajikita katika kuelimisha wananchi namna ya kutumia vifaa vya kujikinga na maambukizi hayo kama vile vifaa vya kusafishia mikono, Gloves na Barakoa (Mask ) za kufunika pua na mdomo.
“ Hili jambo tunapaswa kulichukulia kwa tahadhari kubwa, muwaelimishe wananchi kuhusu namna ya kujikinga na Virusi hivyo, pamoja na kutumia hivyo vifaa ,mnapopita kwenye hayo maeneo hakikisheni kwamba mnawaelimisha vizuri ili wajue ni wakati gani wanapaswa kuvitumia, pia kusafisha miko mara kwa mara” amesema Mhe. Chongolo.
“ Lakini pia tuwasaidie wananchi kutoka kwenye presha waliyo kuwa nayo hivi sasa, tunafahamu kuwa watanzania wengi wamepata taharuki juu ya Vizuri hivi, tusipojitahidi tutajikuta tatizo la presha lina adhiri wananchi kuliko Vizuri vya Corona.
Katika hatua nyingine Mhe. Chongolo amewaeleza viongozi wadini kwamba mikusanyiko isiyokuwa ya lazima haipaswi kuwepo ila kwa ambao wanataka kufunga ndoa wafungishwe lakini kwa kufuata utaratibu ambao utaepusha mikusanyiko ya watu.
Awali Kaimu Mganga Mkuu wa Halmashauri hiyo, John Kijumbe amesema kuwa hadi sasa wameshachukua tahadhari na kama vile kutoa elimu katika maeneo mbalimbali ikiwemo kwa watumishi na wahudumu wa Afya pamoja na kugawa vifaa vya kujikinga na maambukizi ya virusi hivyo.
Hata hivyo Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni imejidhatiti kikamilifu katika kujikinga na virusi hivyo kwakuweka visafisha mikono kwenye mageti yote ya kuingia ikiwa ni katika kuhakikisha kuwa kila mwananchi anayefika kupata huduma mbalimbali wanakuwa salama.