Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mary Makondo akijibu hoja kutoka kwa wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii wakati wa kupokea taarifa ya utekelezaji mradi wa viwanja katika halmashauri ya manispaa ya Ilemela mkoani Mwanza jana
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi Maliasili na Utalii Kemilembe Lwota (wa pili kushoto) akifuatilia uwasilishaji taarifa ya utekelezaji mradi wa viwanja katika halamsahauri ya manispaa ya Ilemela mkoani Mwanza jana. Kushoto ni Waziri wa Ardhi William Lukuvi na kulia ni Naibu wake Dkt Angeline Mabula
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi akifafanua jambo wakati akijibu hoja za baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi Maliasili na Utalii wakati wa kupokea taarifa ya utekelezaji mradi wa viwanja katika halmashauri ya manispaa ya ilemela mkoani Mwanza jana. Kushoto kwa Waziri ni Mwenyekiti wa Kamati Kemilembe Lwota.
Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi Maliasili na Utalii wakifuatilia uwasilishwaji taarifa ya utekelezaji mradi wa viwanja katika halmashauri ya Manispaa ya Ilemela jana mkoani Mwanza. Kulia ni Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mary Makondo.
Wajumbe wa Kamti ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi Maliasili na Utalii wakifuatilia uwasilishwaji taarifa ya utekelezaji mradi wa viwanja katika halmashauri ya Manispaa ya Ilemela jana mkoani Mwanza. (PICHA ZOTE NA HASSAN MABUYE WIZARA YA ARDHI).
*********************************
Na Munir Shemweta, WANMM MWANZA
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imevutiwa na utekelezaji mradi wa kupanga na kupima viwanja eneo la East Buswelu katika kata ya Buswelu na Nyamhongo halmashauri ya Manispaa ya Ilemela mkoa wa Mwanza.
Katika utekelezaji mradi huo, halmashauri ya Manispaa ya Ilemela ilipewa mkopo usio na riba wa shilingi Bilioni 1,550,000,000 na Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa ajili ya kupanga na kupima viwanja 500 na kufanikiwa kuurejesha mkopo huo kwa wakati na kupata faida ya milioni 195,374,000.
Karibu wajumbe wote wa Kamati hiyo waliochangia utekelezaji mradi wa viwanja katika halmashauri ya Manispaa ya Ilemela jana wakati wa kupokea taarifa ya mradi huo walionesha kuridhishwa na kazi nzuri iliyofanywa na watendaji wa halmashauri hiyo chini ya Mkurugenzi wake John Wanga kwa kuitumia vizuri fedha waliyokopeshwa na kuzalisha faida.
Hata hivyo, Mbunge wa Jimbo la Korogwe Timotheo Mzava alishauri faida inayopatikana kutokana na mkopo usio na riba kwa halmashauri nchini itumike katika kazi za ardhi hasa upangaji na upimaji badala ya kutumika katika shughuli nyingine na kutaka kuongezwa kipengele ndani ya mkataba wa mkopo kinachoelekeza suala hilo.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi Maliasili na Utalii Kemilembe Lwota aliipongeza halmashauri ya Manispaa ya Ilemela pamoja na Mbunge wake ambaye ni Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Mkazi Dkt Angeline Mabula kwa kazi nzuri ya kuhakikisha kiasi cha fedha ilichokopeshwa kinatumika vizuri na kuleta matokeo chanya katika halmashauri hiyo.
Kwa mujibu wa Kemilembe, kamati yake inaunga mkono jitihada zilizofanywa na wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuzikopesha halmashauri ili kuongeza kasi ya upimaji ardhi na kubainisha kuwa asilimia kubwa ya ardhi nchini hajapimwa na hivyo kuchangia migogoro ya ardhi.
Kwa upande wake Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi alisema utaratibu ulioanzishwa na wizara yake wa kuzikopesha halmashauri unalenga kuongeza kasi ya upimaji katika halmashauri mbalimbali na hivyo kuzalisha walipa kodi ya pango la ardhi.
Amezitaka halmashauri kutengeneza miradi ya kimkakati na kuandika maandiko yatakayosaidia kupata fedha za mkopo usio na riba na hivyo kuzisaidia katika shughuli zao upangaji, upimaji na umilikishaji ardhi na kuzalisha walipa kodi .
Aidha, Lukuvi alibainisha kuwa, katika kuhakikisha sekta ya ardhi inafanya vizuri zaidi Wizara yake imeanza zoezi la kuwapanga upya wataalamu wa sekta ya hiyo nchi nzima kulingana na uhitaji sambamba na kuanzisha ofisi za mikoa ili kuondoa changomoto za upangaji, upimaji na umilikishaji ardhi nchini.
‘’Kuna baadhi ya halmashauri zina wataalamu wengi wa sekta ya ardhi huku nyingine zikiwa na wataalamu wachache hali hiyo inasababisha shughuli za ardhi katika halmashauri kutofanyika vizuri’’ alisema Lukuvi.
Mbunge wa Jimbo la Ilemela Dkt Angeline Mabula alisema halmashauri ya Manispaa ya Ilemela imekuwa ikifanya vizuri katika zoezi la upangaji, upimaji na umilikishaji ardhi na katika kipindi cha miaka miwili imefanikiwa kupunguza migogoro ya ardhi kwa kiasi kikubwa na kutoa hati 22,185.
Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi nyumba na maendeleo ya Makazi Mary Makondo alisema wizara yake imejipanga kuhakikisha inakabiliana na changamoto ya watumishi kwa kuwapanga katika mikoa yote ishirini na sita ya Tanzania Bara.
Kwa mujibu wa Mary, katika kipindi hiki ambacho idadi ya wataalamu wa sekta ya ardhi hawatoshelezi halmashauri zenye miradi zinaweza kutumia wataalamu kutoka halmashauri nyingine ili kuharakakisha kazi na hivyo kuongeza kasi ya upangaji na upimaji katika maeneo mbalimbali.