Home Mchanganyiko SERIKALI YA AWAMU YA TANO INA DHAMIRA YA DHATI KUONDOA UZEMBE NA...

SERIKALI YA AWAMU YA TANO INA DHAMIRA YA DHATI KUONDOA UZEMBE NA UBADHILIFU MIONGONI MWA WATUMISHI-MHE HASUNGA

0
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akisisitiza jambo wakati wa ufunguzi wa mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara ya Kilimo katika ukumbi wa TPRI Jijini Arusha, leo tarehe 16 Machi 2020. (Picha Zote Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo)
Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Ndg Gerald Kusaya akizungumza kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi kwa ajili ya ufunguzi wa mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara ya Kilimo katika ukumbi wa TPRI Jijini Arusha, leo tarehe 16 Machi 2020.
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb), na Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Ndg Gerald Kusaya wakiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara ya Kilimo katika ukumbi wa TPRI Jijini Arusha, leo tarehe 16 Machi 2020. 
Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Arusha
Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Mhe Rais Dkt John Pombe Magufuli inayo dhamira ya dhati ya kuondoa uzembe na ubadhirifu miongoni mwa watumishi wa umma hivyo ni vyema watumishi wajiepushe na matumizi ya lugha zisizo na staha muda wote wanapotekeleza majukumu yao.
Aidha, serikali imewataka wafanyakazi wote wa Wizara kuendelea kujengewa misingi ya uwajibikaji hasa katika kutambua wajibu wao kwa Umma na kuacha uzembe katika utekelezaji wa majukumu yao huku wakisisitizwa kutumia muda mwingi katika kufanya shughuli ambazo hazina tija zinazoathiri utendaji kazi. 
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) ametoa rai hiyo wakati akifungua mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara ya Kilimo katika ukumbi wa TPRI Jijini Arusha leo tarehe 16 Machi 2020.
Katika mkutano huo ambao wajumbe watapata fursa ya kupokea taarifa ya utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2019/2020 na kujadili na kupitisha makisio ya bajeti ya mwaka 2020/2021 wametakiwa kota Mawazo muhimu katika hatua za utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2020/2021 na kujadili kwa kina na kutoa mapendekezo yatakayosaidia kuboresha bajeti ya Wizara kwa Mwaka ujayo wa fedha.
Amesema kuwa Wizara ya Kilimo inalo jukumu kubwa katika Maendeleo ya nchi hasa kwa kuzingatia kuwa zaidi ya Watanzania asilimia 65.5 wameajiriwa katika kilimo, asilimia 28.7 ya pato la taifa, zaidi ya asilimia 30 ya fedha za kigeni, asilimia 65 ya malighafi za viwanda, asilimia 100 ya chakula chote nchini.  
Pamoja na mambo mengine Waziri Hasunga amewataka wajumbe hao kukumbuka kuwa wizara inawajibika na masuala yote yanayohusu Uendelezaji wa Sekta ya Kilimo hususani; Kuongeza Tija na Uzalishaji wa Mazao ya Kilimo; Kuwezesha Upatikanaji wa Masoko ya Bidhaa za Kilimo; Kuwezesha Uongezaji wa Thamani ya Mazao ya Kilimo; Kuimarisha Mfumo wa Ukusanyaji na Uhifadhi; Uchambuzi na Usambazaji wa Takwimu; Kusimamia Sera, Sheria, Kanuni na Mikakati katika Sekta ya Kilimo; Kuboresha Uratibu katika Sekta ya Kilimo; Kuboresha Uwezo wa Wizara wa kutoa huduma, kuwezesha na kuimarisha Ushirika na Asasi za Wananchi katika Kilimo na Sekta nyingine na Kuzingatia Masuala Mtambuka katika Kilimo.
Mhe Hasunga amesema kuwa katika  kutambua uzito na umuhimu wa majukumu hayo kila mmoja  katika sehemu yake ya kazi anatakiwa kuwajibika na kufanya kazi kwa bidii na kwa  uadilifu ili kuiwezesha Serikali kufikia malengo yake ya kukuza uchumi na kuondoa umaskini kwa wananchi.  
“Aidha, nafahamu kuwa bado tunakabiliwa na changamoto mbalimbali katika utekelezaji wa majukumu yetu ya kutoa huduma kwa umma ikiwemo ukosefu wa rasilimali fedha na rasilimali watu wa kutosha, hali inayosababisha kutofikiwa kwa malengo Niwahakikishie kuwa, Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kutatua changamoto hizo” Alikaririwa Mhe Hasunga 
Ameongeza kuwa, Serikali haitasita kuchukua hatua kwa Mtumishi yoyote atakaye jihusisha na vitendo vya rushwa pamoja na vitendo vinavyokiuka maadili ya Utumishi wa umma.
Kadhalika, Waziri Hasunga amewapongeza watumishi wote wa wizara ya kilimo kwa mafanikio yaliyopatikana kwa Mwaka wa fedha 2019/2020 hivyo amewasihi kujipanga na kuongeza kasi na weledi katika kutekeleza majukumu ya wizara ili Mwaka ujao wa fedha wizara iweze kufikia malengo iliyojiwekea kwa kiwango cha hali ya juu. 
Katika mkutano huo Waziri Hasunga ametangaza kutengua uteuzi wa Kaimu Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Ndg Marko Ndonde kutokana na kushindwa kutekeleza majukumu yake ipasavyo.
Awali akitoa maelezo kuhusu mkutano huo Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Ndg Gerald Kusaya amesema kuwa Mkutano wa baraza la wafanyakazi ni sehemu ya utekelezaji wa Sheria ya Ajira na Mahusiano kazini Na 6 ya mwaka 2004 na Sheria ya majadiliano ya pamoja katika Utumishi wa Umma Na 19 ya mwaka 2003 na Kanuni zake za mwaka 2005
Amesema kuwa Kwa mujibu wa sheria hizo Lengo la kuanzishwa Mabaraza ya wafanyakazi ni kuwa na chombo cha ushauri na majadiliano ya pamoja kati ya wafanyakazi na waajiri ili kuwa na ushirikishwaji mpana wa wafanyakazi mahala pa kazi.