Mnufaika wa Ruzuku inayotolewa na Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini (TASAF), Bibi Albina Matayo, mkazi wa Halmashauri ya Mji wa Babati, Mtaa wa Mrara, akitoa ushuhuda jana kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa wa namna TASAF ilivyomuwezesha kuboresha maisha yake.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapt (Mst) Mhe. George Mkuchika (Mb) akishuhudia kokoto zilizopondwa kwa ajili ya kuuzwa na Bibi Albina Matayo ambaye ni Mnufaika wa Ruzuku inayotolewa na Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini (TASAF), Halmashauri ya Mji wa Babati.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapt (Mst) Mhe. George Mkuchika (Mb) akiwa katika picha na mnufaika wa TASAF, Halmashauri ya Mji wa Babati, Bibi Albina Matayo mbele ya nyumba iliyojengwa na mnufaika huyo kupitia Ruzuku inayotolewa na Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini (TASAF).
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa, Mhe. Dkt. Jasson Rweikiza (Mb), akieleza kuridhishwa na maendeleo ya Mnufaika wa (TASAF), Bibi Albina Matayo, mkazi wa Halmashauri ya Mji wa Babati.
Mbuzi wanaofugwa na Bibi Albina Matayo, mkazi wa Halmashauri ya Mji wa Babati, Mtaa wa Mrara ambaye ni mnufaika wa Ruzuku inayotolewa na Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini (TASAF), ambayo imemuwezesha kuwanunua mbuzi hao.
*****************************
James Mwanamyoto – Babati
Tarehe 15 Machi, 2020
Ruzuku inayotolewa kupitia Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini (TASAF) kwa mnufaika, Bibi Albina Matayo, mkazi wa Halmashauri ya Mji wa Babati, Mtaa wa Mrara, imemuwezesha mama huyo kuendesha biashara ya kuchakata kokoto na kuziuza na hatimaye kuboresha maisha yake kwa kujenga nyumba bora ya bati, ikiwa ni pamoja na kusomesha watoto wake.
Bibi Matayo ametoa ushuhuda huo jana, mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa wakati wa ziara ya kikazi ya kamati hiyo yenye lengo la kukagua utekelezaji wa miradi ya Serikali mkoani
Manyara.
“Ruzuku yangu nimekuwa nikiitumia kupondaponda mawe ili kupata kokoto ambazo nimekuwa nikiziuza kwa shilingi 80,000/= kwa lori moja na kuongeza kuwa, ujira huo umemsaidia kujenga nyumba nzuri ya kuishi na familia yake, kusomesha watoto wake na kufuga mbuzi” Bibi Matayo amefafanua.
Naye, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa, Mhe. Dkt. Jasson Rweikiza (Mb) amesema, kamati yake imejiridhisha pasipo na shaka yoyote kuwa, TASAF imemuwezesha Bibi Matayo kuboresha maisha yake, hivyo ameipongeza TASAF kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kuboresha maisha ya watanzania wenye kipato cha chini.
“Bibi Matayo anayo haki ya kutoa ushuhuda wa faida alizozipata kutokana na TASAF kwani amejenga nyumba nzuri, iliyoezekwa vizuri kwa bati na ameweka mfumo wa umeme kwenye nyumba yake hivyo anasubiria kuingiziwa umeme,” Mhe. Rweikiza ameongeza.
Ruzuku inayotolewa na TASAF katika Halmashauri ya Wilaya ya Babati kwa kiasi kikubwa imewawezesha wanufaika wa mpango huo, kuwekeza katika shughuli za kiuchumi kama vile kilimo, ufugaji wa kuku, bata, mbuzi,
kondoo na kufanya biashara ndogondogo za uuuzaji wa mbogamboga, kugonga kokoto na mama lishe.