Home Mchanganyiko Kituo cha Polisi Mkokotoni kukamilika Mwezi Juni

Kituo cha Polisi Mkokotoni kukamilika Mwezi Juni

0

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni akizungumza mbele ya Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama walipotembelea Mradi wa Ujenzi wa Jengo la Kituo cha Polisi Mkokotoni, kilichopo Kaskazini Unguja, Zanzibar.Kamati hiyo imefika kukagua mradi huo baada ya kituo cha awali kuungua katika ajali ya moto iliyosababishwa na hitilafu za umeme.Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje ,Ulinzi na Usalama, Prosper Mbena, akikagua ukuta wa Mradi wa Ujenzi wa Jengo la Kituo cha Polisi Mkokotoni, kilichopo Kaskazini Unguja, Zanzibar.Kulia ni Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni. Kamati hiyo imefika kukagua mradi huo baada ya kituo cha awali kuungua katika ajali ya moto iliyosababishwa na hitilafu za umeme.Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

*******************************

Na Mwandishi Wetu

Katika kukidhi haja ya Kituo cha Polisi baada ya kituo cha awali kuteketea kwa ajali ya moto, serikali imewakikishia wananchi wa eneo la mkokotoni, Kaskazini Unguja kukamilika kwa mradi huo ndani ya muda wa miezi mitatu  na kuweza kusaidia masuala ya ulinzi na usalama katika maeneo hayo pamoja na maeneo ya kisiwa cha tumbatu ambacho hutegemea huduma ya ulinzi kutoka katika kituo  hicho.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni wakati wa ziara ya Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama walipotembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa kituo hicho cha polisi ambacho ni kituo cha daraja B.

“Katika kuhakikisha tunaendelea kulinda raia na mali zao pamoja na changamoto za ofisi askari wetu wameendelea kufanya kazi katika kituo cha awali na sisi serikali tunaendelea kusimamia kituo hiki kiwe kimekamilika ndani ya miezi mitatu na kiujumla tunaishukuru kamati ya bunge kuja kuona wapi tulikwama ili tukirudi katika vikao vya bunge waweze kulipa msukumo wa kipekee ili mradi huu uweze kukamilika” alisema Masauni

Akizungumza katika ziara hiyo Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje Ulinzi na Usalama, Salum Rehani amesema kamati imefuatilia mradi huo ambao umechukua muda mrefu bila kukamilika na sasa kuna haja ya mradi huo kumaliziwa ili wananchi waweze kufaidi matunda ya ulinzi na usalama.

“Kamati tumekuja kuona mradi ulipogomea na tunashauri mradi huu umaliziwe haraka iwezekanavyo na kuna msukumo maalumu tumepanga na mkandarasi lengo kituo hiki kikamilike maana kubakia bila kukamilika mbeleni italeta matatizo,tunataka wananchi wa maeneo haya wafanye shughuli zao za maendeleo wakiwa na huduma ya ulinzi na usalama ya uhakika” alisema Rehani

Ujenzi wa jingo jipya la Kituo cha Polisi Mkokotoni ulianzishwa baada ya jingo lililokuwa likitumika kama kituo awali kuteketea katika tukio la ajali ya moto kutokana na hitilafu ya umeme iliyosababishwa na miundombinu chakavu ya mfumo wa umeme iliyokuwa katika jingo hilo baada ya kutofanyiwa ukarabati kwa muda mrefu.