Home Mchanganyiko MAJALIWA:MKATABA UJENZI BARABARA NANGANGA-RUANGWA KUSAINIWA MACHI

MAJALIWA:MKATABA UJENZI BARABARA NANGANGA-RUANGWA KUSAINIWA MACHI

0

****************************

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema mwishoni mwa mwezi Machi, 2020 Serikali inatarajia kusaini mkataba wa ujenzi wa barabara ya Nanganga-Ruangwa yenye urefu wa kilometa 50 kwa kiwango cha lami.

Hatua hiyo itawezesha kutatuliwa kwa kero ya changamoto ya miundombinu ya barabara  inayowakabili wananchi wa wilaya ya Ruangwa kwa muda mrefu.

Waziri Mkuu alitoa kauli hiyo jana jioni (Jumamosi, Machi 14, 2020) wakati akizungumza na wananchi wa wilaya ya Ruangwa kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa Wandorwa.

Alisema barabara hiyo ambayo kwa sasa haipo katika hali nzuri itajengwa kwa kiwango cha lami na kwamba Serikali imejipanga katika kuboresha miundombinu ya barabara kwenye maeneo mbalimbali nchini.

Pia, Waziri Mkuu aliwataka wananchi hao washirikiane katika shughuli za maendeleo na kuweka kando itikadi zao za kisiasa kwa sababu maendeleo hayana chama.

 “Mimi nitaendelea kuwatumikia, kuwasikiliza na kuwahudumia, nawaomba tushirikiane na tuweke kando masuala ya itikadi za vyama, huu ni wakati wa kazi ni bora tukashirikiana kufanya kazi kwa maendeleo ya Ruangwa jambo ambalo linawezekana.”

Kwa upande wao, wananchi walitumia fursa hiyo kuishukuru Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuwajali na kwamba ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami ni mkombozi kwao.

Walisema awali katika wilaya yao walikuwa wanakabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwezo za upatikanaji wa huduma za afya, maji na elimu lakini kwa sasa ni historia kwani Serikali ilishazitatua na ilibaki ya barabara ambayo nayo inakwenda kuwa historia.

“Tunamshukuru Rais wetu Dkt. Magufuli kwa upendo wake hasa kwa sisi wanyonge, tunamuombea kwa Mwenyezi Mungu yeye pamoja na wanaomsaidia waweze kutimiza malengo yao yakiwemo na ya ujenzi wa barabara yetu kwa kiwango cha lami.” Alisemma Mwanajuma Chikambo.