************************
Mkuu wa Wilaya ya Gairo Mhe. Siriel Mchembe ameipongeza Kamati ya Usalama Wilaya ya Gairo kwa kufanikisha kuzuia ndoa ya mwanafunzi wa kidato cha kwanza Madege Sekondari. Jina la muoaji ni Bw. Julius Madege Mchyanya wote wanatoka kabila la Wakamba.
Aidha, Mhe. Mchembe amempongeza Kaimu OCD Ndg. Albert Kiwike kwa kusimamia vizuri na kufanikisha zoezi hilo.
Kutokana na uzoefu wa wananchi wanapofanya uhalifu hujihami hasa wanapoona gari la Polisi au la Serikali. Kwa hali hiyo ilibidi gari binafsi litumike.
Hivyo, lilimlazimu OCD kutumia gari binafsi la Askari aliyejitolea (MZALENDO) ambaye ni CPL Revocatus Sabwoya. Pia waliongozana na Askari wa Dawati la Jinsia Bi. Hope Tarimo, Askari wengine na TAKUKURU.
Kwa bahati mbaya wakati wa kurudi kituoni baada ya kuwakamata wahalifu wote; gari hilo aina ya Noah lilisombwa na Maji yaliyoshuka mtoni ghafla wakati wanapambana kuvuka.
Hakuna aliyejeruhiwa ila gari la Askari huyo limeharibika. DC ameagiza gari hilo lipelekwe gereji ili Askari huyo asaidiwe kwenye matengenezo. Anawakaribisha wote wenye mapenzi mema.
Mhe. Mchembe amewaonya wazazi wanaoendekeza ndoa za utotoni. Pia, ameagiza wazazi wa wanafunzi wote ambao hawajaripoti kidato cha kwanza wajisalimishe wenyewe kwenye Ofisi za Watendaji Kata na Vijiji waeleze wanafunzi wako wapi.
Baada ya siku saba wataenda kuelezea Polisi. Kwa sasa ni asilimia 11 ya wanafunzi waliotakiwa kuripoti bado hawajaripoti. Waalimu Wakuu pia wameonywa kwa kushiriki kwenye mipango haramu kwa kuandika utoro wakati wanaujua ukweli. Mwl. Mkuu anatafutwa na Jeshi la Polisi.