Mbunge wa Viti Maalum (CCM) Mkoa wa Singida, Aysharose Mattembe, akitoa zawadi na michango mbalimbali kwa wasichana wa Shule ya Sekondari Mwankoko Manispaa ya Singida.
Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Singida, Aysharose Mattembe akitekeleza moja ya majukumu yake kama mgeni rasmi, kwenye sherehe za siku ya wanawake mkoani hapa.
Mhe. Mattembe, akifurahi pamoja na makundi mbalimbali ya wanafunzi.
-Maandamano ya Wanawake wa Manispaa ya Singida kwenye sherehe ya siku ya wanawake.
Mbunge wa Viti Maalum mkoa wa Singida, Aysharose Mattembe akitekeleza moja ya majukumu yake kama mgeni rasmi, kwenye sherehe za siku ya wanawake mkoani hapa.
Mbunge Mattembe akizungumza.
Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Singida, Aysharose Mattembe, akihutubia wanawake wa mkoa wa Singida waliojitokeza kwenye sherehe za siku ya wanawake juzi.
Na Dotto Mwaibale.
MBUNGE wa Viti Maalum mkoa wa Singida, Aysharose Mattembe akiwa kwenye matukio mbalimbali kuelekea kilele cha siku ya wanawake, aligusa hisia za wengi pale alipoongoza wanawake wenzake kwenda kuwafariji wafungwa wanawake wanaotumikia vifungo vyao kwenge gereza lililopo Singida mjini.
Alionekana kuwa kivutio cha aina yake kwa makundi mbalimbali ya wanawake na hasa wanyonge na wenye uhitaji, huku hotuba zake kabla na wakati wa kilele cha maadhimisho hayo-zikiakisi dhamira ya dhati ya CCM na serikali yake, chini ya Rais Magufuli- kwa muktadha wa Tanzania ya maendeleo.
Mattembe akiwa na wanawake wenzake wa Manispaa ya Singida, waliamini sherehe hizo zisingeweza kwenda vizuri sana kama wasingepata nafasi ya kujumuika kwa pamoja na makundi mengine ya wenzao ambao wapo kwenye matatizo mbalimbali, lengo likiwa ni kuwafariji na kuwafanya wafurahi pamoja.
Siku moja kabla ya maadhimisho hayo, baada ya ziara ya gereza la Singida, Mattembe alikutana na wasichana wa shule ya Sekondari Mwankoko, aliwaasa wasome kwa bidii, waepuke vishawishi ambavyo ndiyo hasa adui mkuu wa ndoto yoyote ile ya mafanikio.
Lakini kabla ya kuwakabidhi vifaa mbalimbali zikiwemo taulo za kike (azma hasa ni kuwasaidia kuhudhuria masomo muda wote kama wavulana hata wakiwa kwenye hedhi) alisisitiza sana na kuwataka wawe na nidhamu, maadili na wajitambue siku zote wawapo shuleni na maeneo ya nyumbani.
Michango na zawadi hizo zilizotolewa na wanawake wa manispaa ya Singida wakiongozwa na Mattembe, lengo lake hasa ni kuweka alama juu ya siku hiyo muhimu ya ‘Wanawake Duniani’ ambayo kwa mwaka huu ina ujumbe unaosema “Kizazi cha usawa kwa Maendeleo ya Tanzania ya sasa na ya baadaye.”
Aidha, akihutubia mamia ya wanawake wa mkoa huo- kama mgeni rasmi wa siku hiyo muhimu- Mbunge Mattembe, huku akishangiliwa alianza kwa kusema kila mwaka serikali nchini inaungana na nchi nyingine duniani kuadhimisha siku hiyo muhimu, ambayo chimbuko lake hasa lilikuwa ni sehemu ya mapambano ya kujenga ujamaa.
Akizungumzia nafasi ya mwanamke katika ushiriki wa uchaguzi mkuu mwaka huu, Mattembe alisema kaulimbiu ya sherehe za wanawake mwaka huu inawahusu, huku akihamasisha wanawake mda utakapofika wasiogope kujitokeza na kuchukua fomu za kugombea nafasi mbalimbali za uongozi.
“Tunapokuwa wengi katika nafasi za uongozi ni rahisi kusukuma mbele mambo na changamoto zinazotuhusu sisi wanawake…lakini jambo hili litawezekana endapo tutapendana, tutashirikiana na kunyanyuana ili tuweze kufikia malengo yetu,” alisema.
Alinukuu moja ya kauli ya Waziri wa Afya wa sasa, Ummy Mwalimu aliyepata kusema siku zote “adui wa mwanamke ni mwanamke mwenyewe, kadhalika na rafiki wa mwanamke pia huwa ni mwanamke mwenyewe”
Kuhusu mikopo ya asilimia 10, Mattembe alikumbusha wanawake kwamba fedha hizo hutolewa bila riba, na ni mkopo sio zawadi au msaada, hivyo kwa anayezipata ahakikishe anapeleka kwenye lengo lililokusudiwa na kuzirudisha ili na wengine nao waweze kukopa.
“Usiporudisha unamzuia mwingine kukopa na ni kosa kisheria. Hizi ni fedha za serikali ambazo lengo lake hasa ni kusaidia kutunyanyua kiuchumi ili tuweze kufikia uchumi mkubwa na hatimaye tuweze kutumia rasilimali hizo kukopa mitaji mikubwa kwenye taasisi za fedha,” alisema Mattembe
Aidha, kuhusu dhana ya usawa na maendeleo, Mattembe alisema azma ya serikali ya awamu ya Tano ni kufikia uchumi wa viwanda ifikapo 2025, na hili haliwezi kufikiwa kama hakuna usawa katika jamii.
“Kwa maana hiyo leo hii watu wa Singida tunaambiwa tubadili fikra zetu zitupelekee kufikia kizazi chenye kuzingatia usawa wa kijinsia ili tupate maendeleo endelevu, mtenge maeneo maalumu kwa ajili ya shughuli za uwekezaji kwa makundi ya wanawake, vijana na wenye ulemavu,” alisema na kuongeza:
“Jamani tutoe huduma kwa kuzingatia usawa, huduma zote zinazotakiwa kwa mwanadamu zinapaswa kutolewa pasipo kuangalia huyu ni mtoto wa kiume au wa kike,” alisema Mattembe.
Alisema daima matendo mema yanayozingatia usawa huleta matokeo chanya kwa maendeleo endelevu ndani ya jamii, lakini kinyume chake husababisha madhara makubwa ikiwemo kuwa chanzo cha unyanyasaji, ubaguzi, mila na desturi potofu ambavyo havina tija wala maadili mema ndani ya jamii
Alisema tafsiri ya kizazi cha usawa hakina maana ya wanawake pekee, bali ni humaanisha hali ya kutokuwa na ubaguzi na upendeleo kwa makundi yote kwenye jamii, kwa maana ya wanaume, wanawake, vijana, watoto na wenye ulemavu.
Inasikitisha kuona mpaka sasa wapo watoto wa kiume ambao bado wananyimwa fursa yao muhimu ya kwenda shule kwa kuendelea kuchunga mifugo, huku akirudia mara kadhaa kusisitiza kwamba hii haikubaliki na huo ni unyanyasaji wa kijinsia.