Mstahiki Meya Mstaafu wa Jiji la Arusha Kalist Lazaro akiongea na vyombo vya habari leo leo jijini Arusha
Na Ahmed Mahmoud Arusha
CHAMAcha Mapinduzi,CCM, hakitatumia dola kubakia madarakani bali kitaitumia dola katika kuwatumikia na kuwahudumia wananchi kwa kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo na kuboresha huduma za jamii.
Hayo yameelezwa leo jijini Arusha kwenye ukumbi wa Hotel ya Arusha Palace, na aliyekuwa Meya wa Jijiji la Arusha,Kalisti Lazaro,alipokuwa akitolea ufafanuzi kauli ya Katibu mkuu wa ccm taifa Dakta Bashiru Ally aliyoitoa wiki iliyopita alipokuwa akizungumza na vyombo vya habari vinavyomilikiwa na kampuni ya IPP ya Jijini Dar es Salaam.
Kalisti,ambae amejiunga na Chama cha Mapinduzi,CCM,mwaka jana akitokea Chadema, amesema kuwa Katibu mkuu aliposema kuwa Chama kilichoko madarakani kikiondolewa kwenye uchaguzi mkuu ni uzembe unaotokana na kushindwa kuitumia dola hakumaanisha kwamba chama hicho kitatumia dola kusalia madarakani.
Amesema katibu mkuu alimaanisha kwamba ccm ikishinda itatumia serikali kuwahudumia wananchi na sio kuwakandamiza kama wanavyodai.
Kalisti,amesema viongozi wa Vyama vya Siasa nchini wanapotosha kauli hiyo na kudai kuwa Chama cha mapinduzi kitatumia dola kuuminya na kuukandamiza upinzani jambo ambalo sio kweli .
Amesema kuwa Vyama vyote nchini mwaka 2015 viliingia kwenye mchakato na ccm iliibuka mshindi na hapakuwepo na matumizi mabaya ya dola hivyo wasipotoshe bali waeleze ukweli tu
Na pia mwaka huu ni mwaka wa uchaguzi mkuu hivyo kila Chama kitaingia majukwaani kuomba ridhaa ya wananchi na Chama kitakachoshinda kitaunda serikali.
Kuhusu maadhimisho ya siku ya wanawake Ulimwenguni yaliyoadhimishwa Marchi 9 mwaka huu kwenye uwanja wa mpira wa Shekh Amri Abeid ,Jijini Arusha ,Kalisti ,amesema yalikuwa ya mafanikio makubwa.
Ameipongeza halmashauri ya Jijiji la Arusha, kwa kufanikisha maadhimisho hayo yaliyoshirikisha wanawake wote wa Jiji la Arusha ,wakiwemo madiwani wa Vyama vyote vya siasa bila kujali itikadi .
Amesema maadhimisho hayo yamebeba sura ya kitaifa, hivyo yasigeuzwe kuwa ya kichama kama yalivyofanyika katika mkoa wa Dar es Salaam,ambapo Chama kimoja cha kisiasa kilifanya maadhimisho hayo kichama jambo ambalo sio sahihi.
Amesema kuwa maadhimisho hayo ambayo yanatimiza miaka 25 yanalenga kuwaunganisha wanawake wote pamoja katika kudai haki zao na kamwe yasigeuzwe kuwa ya kisiasa.