Wajumbe wakipeana mikono mara baada ya kikao baina ya wizara na kampuni ya Noble Helium kwisha.
Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Profesa Shukrani Manya (kulia) akibadilishana mawazo na wager Jennines baada ya kikao baina ya wizara na kampuni ya Noble Helium kuhitimishwa.
Waziri wa madini, Doto Biteko (mbele), Naibu waziri, Stanslaus Nyongo ( kushoto) na Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Profesa Shukrani Manya (kulia) wakijadili jambo mara baada ya kikao baina ya wizara na kampuni ya Noble Helium kuhitimishwa.
Waziri wa Madini, Doto Biteko akiagana na wajumbe walioshiriki kikao baina ya wizara na kampuni ya Noble Helium mara baada ya kuhitimisha kikao hicho.
Justyn Wood (katikati) akieleza mada wakati wa kikao baina ya kampuni anayoisimamia na wizara.
Na Nuru Mwasampeta, Dodoma
Waziri wa Madini, Doto Biteko leo Machi 10, 2020 amekutana na Wawekezaji wa Kampuni ya Uchimbaji Madini ya Helium ya Noble Helium na kuitaka kuharakisha Utekelezaji wa mradi huo.
Biteko aliongeza kuwa hakuna serikali duniani isiyohitaji wawekezaji na hivyo basi kutokana na umuhimu na uhitaji wa wawekezaji nchini ni vema wawekezaji kwenda na kasi ya serikali husika ili kupelekea malengo yaliyowekwa na nchi kufikiwa ikiwa ni pamoja na kukuza uchumi wa nchi.
Wawekezaji hao walipata leseni ya utafiti wa madini hayo katikati ya mwaka jana (2019) na hivyo kuamua kufika katika Ofisi ya Waziri Biteko ili kueleza hatua waliyofikia katika utafiti wa madini hayo.
Akizungumzia uhakika wa uwepo wa madini hayo nchini, Justyn Wood mmoja wa wajumbe kutoka kampuni ya Noble Helium, amesema kwa hatua za awali na kwa namna miamba ilivyokaa na jiolojia ya mahala wanapofanyia kazi wana uhakika mkubwa wa uwepo wa kiasi kikubwa cha madini hayo.
Wengine waliohudhuria kikao hicho ni pamoja na Viongozi Waandamizi wa wizara pamoja na Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Profesa Shukrani Manya na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST), Dkt. Daniel Budeba.