SERIKALI wilaya ya Arusha,imesema kuwa imejipanga ili kuondoa na kukomesha vitendo vya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia dhidi ya wanawake na wasichana ambavyo huzima ndoto na matarajio yao katika maisha .
Mkuu wa wilaya ya Arusha,Gabriel Daqarro, ameyasema hayo leo alipokuwa akizindua kongamano la maadhimisho ya siku ya wanawake Ulimwenguni iliyofanyika uwanja wa mpira wa Sheikh Amri Abeidi,Jijijini Arusha.
Mkuu wa wilaya, amesema kuwa bado kuna vitendo vya ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na wasichana na kueleza kuwa Serikali itaunganisha nguvu zake na mashirika yasiyo ya kiserikali katika kukomesha ukatili wa kijinsia na kuchukua hatu pindi inapolazimika
Amesema chimbuko la kudai haki na usawa wea kijinsia lilianzishwa na wanawake nchini Marekani mwaka 1919 walipodai haki zao kutokana na kulipwa ujira mdogo, kunyanyaswa kiuchumi ,kisiasa na kijamii .
Amesema usawa wa kijinsia kwenye Jamii zetu unaathiriwa na maswala mbalimbali ya kijamii hasa wasichana ambao wapo shuleni ndio wahanga wakubwa wa vitendo vya ukatili wa kijinsia ambavyo kuzima ndoto na matarajio yao katika masomo na matokeo yake wanapata mimba.
Amesema kuwa serikali itaendelea kuwalinda wanawake na wasichana kwa kuimarisha Dawati la Jinsia katika Jeshi la Polisi,ambapo litawachukulia hatua stahiki wale wote watakaowakaojihusisha na vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na wasichana.
Pia amesema kuwa katika mwendelezo huo wa kumlinda wanafunzi wa kike, Afisa elimu, Waratibu elimu kata pamoja na watendaji wa kata wanaenda kutembelea shule mbalimbali na kutoa elimu ya kuwalinda wasichana dhidi ya vitendo vya ukatili .
Aidha ameitaka ofisi ya mkurugenzi wa halmashauri ya Jiji kuwakamata watoto wanauuza mifuko kwenye masoko ambao wameacha shule na kuwarejesha shuleni ili waendelee na masomo yao.
Awali Grace Murro,kutoka shirika la World vision , akiwasilisha taarifa ya utafiti wa ukatli wa kijinsia kwa wanafunzi kwenye shule za sekondari, amesema kuwa kuna manyanyaso ambapo walimu wa masomo ya Biolojia huwa wanatumia lugha za uzalilishaji kwa wasichana.
Amesema baadhi ya walimu wa kike huwa wanatumia lugha za kuwadharirisha wasichana na hivyo kuwaondoa kwenye hali ya masomo na kusababisha kukosa usikivu na kusisitiza kuwa kiwango cha ukatili ni kikubwa kwenye shule za sekondari hivyo kukwamisha ndoto za wasichana kuendelea na masomo.