*************************
Na Mwandishi Wetu
Naibu waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana na Ajira na wenye Ulemavu, Mhe. Antony Mavunde, ameitaka menejimenti ya Wakala wa Usalama na afya Mahali pa Kazi (OSHA) kuendelea kujenga uwezo wa watumishi wake ili kuwawezesha kutekeleza majukumu yao kwa weledi zaidi.
Ametoa agizo hilo wakati akifungua kikao cha sita cha baraza la tatu la wafanyakazi wa OSHA kilichofanyika kwa siku moja katika Hoteli ya Gold Crest jijini Arusha na kufuatiwa na mafunzo ya kujiandaa kustaafu, kujikinga na magonjwa yanayoambukiza mfano UKIMWI na virusi vya Korona pamoja Misingi ya Kazi mahali pa kazi.
“Mchango wa taasisi ya OSHA katika kufanikisha sera ya nchi yetu ya uchumi wa viwanda ni mkubwa mno kwani viwanda vinaambatana na vihatarishi mbali mbali vya kiusalama na afya hivyo kuendelea kujenga uwezo wa wakaguzi wetu wa usalama na afya mahali pa kazi
ni jambo la msingi sana,” alisema Mh. Mavunde na kuongeza:
“Kuna mabadiliko mengi sana yanayotokea hususan katika teknolojia hivyo ili kuendana na kasi ya mabadiliko hayo hatuna budi kuwaendeleza wataalam wetu kiujuzi mara kwa mara. Hii itawawezesha kutekeleza majukumu yao kwa weledi na hatimaye kuleta tija katika uzalishaji.”
Aidha, Mh. Mavunde aliwataka OSHA kuwekeza zaidi katika kuwaelimisha wananchi kuhusu masuala ya afya na usalama kazini kwani wengi wao bado hawana ufahamu wa kutosha wa masuala hayo muhimu.
Hata hivyo, Naibu Waziri huyo ameipongeza OSHA kwa kazi nzuri inayofanyika katika ukaguzi wa usalama na afya kwenye maeneo ya kazi nchini, kutoa huduma bora
zinazowaridhisha wateja na hivyo kuondoa malalamiko ambayo yalikuwa yakijitokeza miaka ya nyuma na hivyo kuwataka kuongeza jitihada zaidi katika kuwahudumia watanzania.
Kwa upande wake Kaimu Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi Khadija Mwenda, amesema miongoni mwa agenda za kikao hicho ni kujadili rasimu ya Mpango Mkakati wa taasisi wa
miaka mitano ijayo (2020/2021-2024/2025 ambao baadhi ya malengo yake ni kusajili maeneo mengi zaidi ya kazi na kuhakikisha kwamba yanakidhi viwango vya usalama na
afya mahali pa kazi.
“Tukiwa tunamalizia kutekeleza Mpango Mkakati unaoishia mwaka huu wa fedha (2019/2020), tuliona ni muhimu kufanya tathmini ili kubaini changamoto au ombwe lililokuwepo katika mpango huo ambapo tathmini hiyo ndiyo imetuwezesha kuja na Mpango Mkakati mpya unaotatua changamoto zilizobainika,” alieleza Mwenda.
Kikao hicho cha baraza la wafanyakazi wa OSHA ni matokeo ya Sheria Na. 19 ya Mabaraza ambayo inazitaka taasisi mbali mbali kuunda mabaraza hayo ili kuleta
ushirikishwaji katika utendaji wa taasisi husika.