Wafanyakazi wa TANESCO Mkoa wa Morogoro wakisheherekea siku ya Wanawake Duniani katika viwanja vya Jamuhuri Manispaa ya Morogoro
………………………………………………………………………………………………………..
NA FARIDA SAIDY,MOROGORO
Jamii imeaswa kusaidia watu wenye uhitaji wakiwemo walioko magerezani hususani wanawake kwa kuwa bado wanauhitaji wa vitu mbalimbali kama binaadamu wengine walioko uraiani.
Wito huo umetolewa na meneja wa TANESCO Mkoa wa Morogoro Mhandisi Fedgrace Shuma baada ya kutembelea gereza la wanawake la kingorwuila lililopo Manispaa ya Morogoro,akiambatana na wafanyakazi wanawake wa TANESCO na kutoa msaada ya vitu mbalimbali ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha siku ya wanawake duniani ambayo hufanyika March 8, kila mwaka.
Vitu vilivyotolewa na wafanyakazi wanawake wa TANESCO ni pamoja na taulo za kike,mafagio,nguo za ndani,makwanja,sabuni,ndala pamoja na mafuta ya kupaka ambavyo vyote vikiwa na thamani ya shilingi milioni moja na laki tano za kitanzania.
Hata hivyo amesema kuwa wao kama TANESCO wameamua kusheherekea siku ya wanawake duniani kwa kurudisha fadhila kwa jamii kwa kutoa msaada kwa warekebishwa wa gereza hilo.
Aidha amewataka wanawake kushiriki katika mambo mbalimbali ya kiuchumi ili kujikwamua kimaisha na kuachana na dhana ya potofu ya kuamini kuwa kuna baadhi ya kazi zinafanywa na wanaume pekee.
Maadhimisho ya Siku ya Wanawake kitaifa yamefanyika katika mkoa wa Simiyu yakiwa na Kauli Mbiu isemayo Kizazi cha Usawa kwa Maendeleo ya Tanzania ya Sasa na Baadaye.