Mkazi wa Kijiji cha Isoliwaya wilayani Kilolo mkoani Iringa, Vitolina Mbweli akipokea simu mpya ya mkononi kutoka kwa Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye alipofika kuzindua mnara wa mawasiliano kijijini hapo. Simu hiyo imenunuliwa na Mbunge wao wa Kilolo, Venance Mwamoto (wa kwanza kushoto)
Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye akizungumza na wanakijiji wa Isoliwaya (hawapo pichani) wilayani Kilolo, Iringa kabla hajazindua mnara wa mawasiliano. Wa kwanza kulia ni Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote, Justina Mashiba na wa pili kushoto ni Mbunge wa Kilolo, Venance Mwamoto
***************************
Na Prisca Ulomi, WUUM, Iringa
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imepiga marufuku kwa mwananchi yeyote kumsajilia laini ya simu ya mkononi kwa alama ya vidole kwa kutumia kitambulisho cha taifa cha NIDA mtu mwingine kwa kuwa kufanya hivyo ni kosa la kisheria.
Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye kwa waandishi wa habari wa mkoa wa Iringa wakati akiwa kwenye mikutano ya hadhara kwenye kijiji cha Idodi na Isoliwaya mkoani humo wakati akizindua minara ya mawasiliano kwenye kata ya Idodi, Kihesa na Ihimbo zilizopo wilayani Kilolo na Iringa mjini.
Nditiye amesema kuwa ni marufuku kwa mwananchi yeyote kumsajilia laini ya simu ya mkononi mtu mwingine kwa alama ya vidole kwa kutumia kitambulisho cha taifa cha NIDA hata mtu huyo akiwa ni mkeo au mumeo kwa kuwa kwa kufanya hivyo ni kosa kisheria kupitia sheria zinazosimamiwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).
Amefafanua kuwa Serikali imebaini kuwa kumeibuka tabia kwa baadhi ya wananchi kuwasajilia laini za simu watu wengine kwa kisingizio kuwa hawajapata namba au
kitambulisho cha taifa cha NIDA ambapo amesema kuwa tayari Serikali imetoa namba hizo au vitambulisho hivyo kwa wananchi wengi kwenye maeneo mbali mbali nchini.
Pia, amesema kuwa Serikali iliongeza muda wa kuzima laini za simu ambazo wahusika hawajazisajili kwa alama za vidole kwa kutumia kitambulisho cha taifa cha NIDA ili
kuhakikisha kuwa wananchi walio na laini hizo wanakamilisha zoezi la usajili kwa kutambua umuhimu wa huduma za mawasiliano na matumizi ya simu za mkononi kwa kuwa hivi sasa wananchi wanatumia simu kwa shughuli mbali mbali ikiwemo za kiuchumi na kijamii.
“Ujue kitambulisho kinachotumika kusajili laini ya simu kwa alama za vidole ni kimoja tu ambacho ni kitambulisho cha taifa cha NIDA na kinatolewa na Serikali kwa mtu mmoja tu, kama kuna kosa linatokea la matumizi mabaya ya mawasiliano na laini yako ndio imetumika kwa kuwa ni kitambulisho chako kimetumika, sisi tunaifunga hiyo laini na hutasajili tena, mwananchi nenda kwa kampuni ya simu iliyokusajili ili kuhakikisha na kujiridhisha laini ulizosajili na sio vinginevyo,” amesisitiza Nditiye.
Naye Mkuu wa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini wa TCRA, Mhandisi Asajile John amesema kuwa wanaendelea kushirikiana na kampuni za simu za mkononi kusajili laini
za simu za mkononi kwa alama za vidole kwa kutumia kitambulisho cha taifa cha NIDA ambapo hadi sasa asilimia 81 ya laini zimesajaliwa na kwa waliobaki wanaendelea
kusajiliwa kwa wale walikuwa na laini hizo tangu hapo awali na zoezi litakuwa endelevu kwa wanaochukua laini mpya.
Amewataka wananchi kuzingatia sheria na kanuni zinazosimamia na kuendesha huduma za mawasiliano kwa kuwa mawasiliano yanatumika kwa shughuli za kiuchumi,
kijamii na kisiasa hivyo wananchi wajiepushe kutumia mawasiliano hayo vibaya ili waendelee kunufaika na huduma za mawasiliano.
“Mwezi Desemba mwaka 2019 kulikuwa na akaunti za benki kwenye mitandao zipatazo milioni 25 kwenye simu za mkononi na katika kipindi hicho miamala milioni 248 ilifanyika na miamala hiyo ilikuwa na jumla ya thamani ya shilingi trilioni 9.5 na zote kwa ujumla wake zinaonesha umuhimu wa Sekta ya Mawasiliano kwenye uwezeshaji wa kiuchumi ili kufikia uchumi wa kati,” amefafanua Mhandisi Asajile.
Aidha, Nditiye ametoa rai kwa mawakala wote wa kampuni za simu za mkononi nchini kuwasaidia wananchi kusajili laini za simu zao kwa alama za vidole kwa kutumia
kitambulisho cha taifa cha NIDA kwa kuzingatia maelekezo wanayopatiwa na TCRA.