Mkurugenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Paul Rwegasha (wa kwanza kulia), akiwasilisha taarifa fupi ya Jengo la Tatu la Abiria la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA-TB3), kwa Bodi ya Ushauri (MAB) ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), ilipotembelea jengo hilo leo.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Mhandisi Mshauri Julius Ndyamukama (aliyenyanyua mikono) akielezea jambo mbele ya Bodi ya Ushauri (MAB) iliyotembelea jengo la Tatu la abiria la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA-TB3) katika ziara ya kikazi.
Kaimu Meneja wa Jengo la Tatu la Abiria la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA-TB3), Mhandisi Barton Komba (kulia), akitoa maelezo mbalimbali kwa Bodi ya Ushauri (MAB) iliyotembelea jengo hilo leo. Aliyevaa tai ni Mwenyekiti wa Bodi hiyo Dkt. Masatu Chiguma.
Wajumbe wa Bodi ya Ushauri (MAB) ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), wakiangalia ramani ya jengo hilo wakati wakilitembelea katika ziara ya kikazi iliyofanyika leo.
Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri (MAB) ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Dkt Masatu Chiguma akipimwa joto la mwili na Afisa Afya, Yusta Malisa wakati bodi hiyo ilipotembelea Jengo la Tatu la Abiria la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA-TB3), kwa ziara ya kikazi.
Wajumbe wa Bodi ya Ushauri (MAB) ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), wakiangalia moja ya begi likipita kwenye mkanda ikiwa ni hatua ya tatu kwa ukaguzi kabla halijafika hatua ya mwisho tayari kupelekwa kwenye ndege, walipotembelea jengo hilo leo katika ziatra ya kikazi.
…………………………………………………………………………………
Na Bahati Mollel,TAA
BODI ya Ushauri (MAB) ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), imeridhishwa na ukaguzi wa abiria wanaotoka nje ya nchi wanaotumia Jengo la Tatu la Abiria la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA-TB3).
Mwenyekiti wa MAB, Dkt Masatu Chiguma amesema leo mara baada ya kumalizika kwa ziara yao ya kwanza ya kikazi tangu kuteuliwa kwao hivi karibuni ya wametembelea jengo hilo kuwa maafisa afya waliopo kwenye Jengo hilo wanafanya ukaguzi kulingana na taratibu zilizowekwa, ili kuzuia maambukizi ya Homa Kali ya mapafu inayoambukizwa na virusi aina ya Corona, isiingie nchini.
Dkt Chiguma amesema tahadhari ya kuzuia ugonjwa huo ulioanzia nchini China na kusambaa kwenye nchi mbalimbali Duniani, imefanyika ipasavyo kwenye Jengo hilo, baada ya kulitembelea na kuona, vifaa na utendaji wa watumishi hao wa afya.
“Matayarisho ya kujihadhari na huu ugonjwa wa Corona yamefanyika kwa hali ya juu na wajumbe wa Bodi tumeridhika baada ya kuona vifaa vinavyohitajika kuvaliwa na watendaji wa kitengo cha afya na pia watumishi wa TAA waliopo maeneo ya kuwasili na maeneo mengine,” amesema.
Akizungumzia jengo hilo, Dkt Chiguma amesema anaipongeza serikali kwa ujenzi wa jengo hili la kisasa lenye vifaa vya kimataifa, ambapo uendeshaji wake ni wa hali ya juu.
“Tumepita kuanzia mwanzo wa jengo hadi mwisho wa jengo na tumejionea namna lilivyo bora na zuri, hata vifaa vyake ni vya kitaalam sana, ukiangalia eneo la mizigo ni mashine tu zinafanyakazi pamoja na kuwa na Watumishi wachache lakini kila kitu kinaongozwa na mashine za kisasa,” amesema.
Hatahivyo, amesema Bodi imebaini bado katika jengo hili kuna upungufu mkubwa wa watumishi, ambapo sasa waliopo wengi ni wanaofanya kazi kwa mikataba mifupi na wale wanaendelea kujifunza (Internship), ambapo ni hatari kwa kuwa sio wakutegemewa zaidi kutokana kuweza kuondoka wakati wowote watakapopata ajira ya kudumu.
Pia ameitaka menejimenti ya TAA kuhakikisha inaboresha maslahi ya watumishi ili waendelee kulitunza jengo hilo kwa kufanya kazi kwa bidii.
Halikadhalika amesema ulinzi na usalama wa abiria na mizigo yao kwenye Jengo hilo ni wa hali ya juu na uliopangiliwa vyema, kwa kuanzia abiria anapoingia wakati akisafiri hadi kufika kwenye ndege, hata mizigo inavyokaguliwa kwa kupitia hatua tano napo panaridhisha.
Katika hatua nyingine, Dkt Chiguma amewaita Watanzania kujitokeza kwa wingi kuwekeza kwenye jengo hilo, pale TAA itakapotangaza zabuni mbalimbali, maana bado yapo maeneo mengi ya uwekezaji.
Awali akiwasilisha ripoti ya ujenzi wa jengo hilo, Mkurugenzi wa JNIA, Paul Rwegasha amesema wanakabiliwa na changamoto ya gharama kubwa za uendeshaji, ambapo jengo zima kwa asilimia 100 linatumia umeme wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), na ukikatika hutumika jenereta ambazo zinatumia mafuta mengi.
Pia amesema wanakabiliwa na upungufu wa watumishi, ambapo wanalazimika kutumia zamu fupifupi na wengine waliotoka asubuhi kurudi jioni kuongeza nguvu (supporting).