Home Biashara Uchumi wa Tanzania Kuendelea Kupaa katika kipindi kifupi kijacho’ Wataalam IMF

Uchumi wa Tanzania Kuendelea Kupaa katika kipindi kifupi kijacho’ Wataalam IMF

0

Na.Mwandishi  Maalum – Dar es Salaam

Jitihada za makusudi za Serikali ya Awamu ya Tano katika kusimamia na kutekeleza sera madhubuti za fedha na uchumi hasa katika kusimamia ukusanyaji wa mapato na matumizi, kupunguza matumizi yasiyo ya lazima, pamoja na usimamizi wa Benki, zimeelezwa kuwa ni miongoni mwa vitu vilivyoifanya Tanzania kukua kiuchumi na kunakoisaidia kue ndelea na ukuaji wa kasi katika siku zijazo.

Kwa mujibu wa ripoti ndogo iliyotolewa Jijini Dar es Salaam na wataalam wa Shirika la Fedha Ulimwenguni (IMF), waliomaliza muda wao wa kufanya utafiti hapa nchini kuanzia tarehe 20 Februari hadi Machi 4 Mwaka huu, Tanzania ni miongoni mwa nchi chache za Afrika zinazofanya vizuri katika ukuaji wa Uchumi.

Kiongozi wa timu hiyo ya IMF iliyotembelea Tanzania Enrique Gelbard  amesema kiwango cha ukuaji wa uchumi katika kipindi cha miezi michache iliyopita kinaonyesha ukuaji wa kasi kutokana na uwekezaji mkubwa unaofanywa na serikali , kuongezeka kwa mauzo ya nje ya nchi, pamoja na kuongezeka kwa mikopo kwa sekta binafsi.

Amesema viashiria hivyo vitaifanya Tanzania kuendelea kukua kiuchumi katika siku zijazo katika sekta za Ujenzi na madini, unaosaidiwa na kupungua kwa mfumuko wa bei kwa kiwango cha asilimia 3.7 pamoja na kuimarika kwa viwango vya kubadilisha fedha za kigeni ,kadhalika na uwepo wa akiba ya kutosha ya fedha za kigeni inayoweza kufanya manunuzi kwa kipindi cha takribani miezi mitano.

Aidha mtaalam huyo amezungumzia kuimarika kwa uchumi hapa nchini kuwa kumesababishwa na sera madhubuti za usimamizi wa fedha ambazo zimeleta mageuzi makubwa ya kiuchumi hapa nchini, pia amezipongeza mamlaka husika kwa kuendelea kusimamia ukusanyaji wa mapato.