Meneja wa Huduma Jumuishi za Fedha wa BoT, Bi. Nangi Massawe, akizungumza na waandishi wa habari katika mkutano uliofanyika Benki Kuu ya Tanzania Septemba 17, 2026.
…………
Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imeeleza kuwa imeweka mikakati mbalimbali kuhakikisha wanawake na watu wenye ulemavu wanapata huduma rasmi, salama na zenye manufaa za kifedha, hatua ambayo imechangia Tanzania kutambuliwa na kupata tuzo kutoka Umoja wa Kimataifa wa Huduma Jumuishi za Fedha (AFI).
Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu tuzo hizo, Meneja wa Huduma Jumuishi za Fedha wa BoT, Bi. Nangi Massawe, amesema AFI ni jumuiya ya kimataifa inayojumuisha benki kuu, wadhibiti wa sekta ya fedha na wizara za fedha kutoka nchi zinazoendelea, ikiwa na wanachama kutoka nchi 84.
Amesema tangu kuanzishwa kwake, AFI imekuwa chombo muhimu cha kubadilishana uzoefu, kuweka sera na kufuatilia hatua zinazochukuliwa na nchi wanachama katika kuongeza ushiriki wa wananchi katika mfumo rasmi wa fedha.
Massawe amesema Tanzania imepata tuzo ya kwanza katika kipengele cha Maya Declaration Award, ambacho hutambua nchi au taasisi zilizofikia malengo na ahadi walizojiwekea katika kuendeleza huduma jumuishi za kifedha.
Amesema Tanzania iliweka jumla ya ahadi 13 chini ya mpango huo na imefanikiwa kutekeleza sita, huku hatua nyingine zikiendelea kufanyiwa kazi kulingana na mikakati iliyowekwa.
Miongoni mwa mafanikio yaliyotajwa ni Tanzania kufanikiwa kuandaa na kutekeleza Mkakati wa Taifa wa Huduma Jumuishi za Fedha, ambapo kwa sasa nchi iko katika utekelezaji wa mkakati wa tatu, unaotekelezwa kwa kipindi cha mwaka 2023 hadi 2028.
Massawe amesema mkakati huo umeweka kipengele maalumu cha jinsia kwa lengo la kupunguza pengo kati ya wanawake na wanaume katika upatikanaji na matumizi ya huduma za kifedha, pamoja na kuhakikisha wanawake wanapata bidhaa na huduma zinazozingatia mahitaji yao.
Amesema hatua nyingine zilizochukuliwa ni kushughulikia changamoto zinazowakabili wanawake katika huduma za kifedha, ikiwemo vikwazo vya nyaraka, gharama za huduma za kidijitali na mahitaji ya dhamana wakati wa kupata mikopo.
Ameeleza kuwa BoT pia imeweka mkazo katika matumizi ya takwimu zilizogawanywa kwa jinsia ili taasisi za fedha ziweze kufahamu kwa usahihi kiwango cha wanawake na wanaume wanaopata na kutumia huduma za kifedha na kupanga hatua zinazofaa.
Katika eneo la watu wenye ulemavu, Massawe amesema Tanzania imeanza kuweka mikakati mahsusi ya kuhakikisha kundi hilo linapata huduma za kifedha kwa kuzingatia mahitaji yao, hatua ambayo pia imekuwa sehemu ya utekelezaji wa ajenda ya huduma jumuishi za kifedha.
Amesema BoT imeendelea kushirikiana na wadau kupitia Baraza la Taifa la Huduma Jumuishi za Fedha, likiongozwa na Benki Kuu, ili kuhakikisha mikakati na sera zinazowekwa zinawafikia wananchi na makundi yenye changamoto katika kupata huduma za kifedha.
Massawe amesema juhudi hizo zimechangia kuongezeka kwa kiwango cha ujumuishi wa kifedha nchini kutoka asilimia 65 mwaka 2017 hadi asilimia 76 mwaka 2023, huku vipimo vya kati vikionyesha kuwa kiwango hicho kimeendelea kuongezeka.
Amesema pia pengo la huduma za kifedha kati ya wanawake na wanaume limepungua kutoka asilimia 10 mwaka 2017 hadi asilimia 3.6 mwaka 2022, huku hatua zaidi zikiendelea kuchukuliwa kulipunguza.
Amesema utambuzi huo kutoka AFI unaakisi hatua zilizochukuliwa na Tanzania katika kutekeleza ahadi na mikakati ya huduma jumuishi za kifedha, ikiwemo kuongeza ushiriki wa wanawake, watu wenye ulemavu na makundi mengine katika mfumo rasmi wa fedha.
