Home Mchanganyiko MBUNGE TUNDURU KUSINI ATUMIA MILIONI 485 KWA AJILI YA MAENDELEO TUNDURU

MBUNGE TUNDURU KUSINI ATUMIA MILIONI 485 KWA AJILI YA MAENDELEO TUNDURU

0

Mbunge wa jimbo la Tunduru Kusini Daimu Mpakate kulia akiongea na wakazi wa kijiji cha Chiwana kata ya Chiwana Wilayani Tunduru jana katika mkutano wa Hadhara ambapo alitoa shilingi ml 12 kwa ajili ya ujenzi wa matundu  ya vyoo na ukarabati wa vyumba vya madarasa kwa baadhi ya shule za msingi katika kata hiyo.

Picha na Mpiga Picha Maalum

…………………………………………………………………………………………..

Na Mwandishi Wetu

MBUNGE wa jimbo la Tunduru Kusini Daimu Mpakate,amewataka wakazi wa kijiji cha Chiwana kata ya Chiwana wilayani Tunduru,kuwa walinzi wa  miradi  inayoendelea kutekelezwa  na Serikali ya awamu ya tano katika vijiji mbalimbali ili kurahisisha upatikanaji wa huduma za kijamii.

Mpakate alisema hayo jana, wakati akikabidhi msaada wa shilingi milioni  12 ambapo shilingi  ml 6 zitatumika kwa  ajili ya ujenzi wa matundu ya vyoo  na ukarabati wa baadhi ya vyumba vya madarasa katika shule ya msingi Chiwana.

Alisema, maendeleo yanaletwa kwa ushirikiano kati ya Serikali,wananchi na wadau wengine  katika kufanikisha mahitaji muhimu katika jamii badala ya kuiachia Serikali pekee yake.

“Mheshimiwa diwani na wananchi mimi kama Mbunge nitaendelea kuboresha miundombinu ya shule,Afya na maji katika jimbo letu,hii shule ndiyo iliyobeba jina la kata ya Chiwana,kwa hiyo ni lazima sisi viongozi  tuhakikishe tunaelekeza nguvu kubwa  hapa”alisema Mpakate.

Alisema, yeye kama Mbunge wa jimbo hilo  ametumia zaidi ya Ml 485 kwa ajili ya  kusaidia Utekelezaji wa miradi ya maendeleo, kati ya fedha hizo asilimia 80 zimetumika kuimarisha na kuboresha miundombinu ya elimu  katika kipindi cha miaka minne 2015-2019.

Aidha alieleza kuwa, katika kipindi hicho amefanikiwa kufunga mashine za kusaga nafaka, kusambaza vitabu vya masomo mbalimbali vyenye thamani ya ml 32, kwa shule za sekondari,kugawa bati 6000,saruji mifuko 12,000 vifaa ambavyo vimetumika kwa ajili ya ujenzi wa ofisi za Serikali za vijiji,kata na sekta ya Afya katika vijiji mbalimbali katika jimbo la Tunduru kusini.

Mpakate alisema, fedha hizo  zimekwenda kutekeleza miradi iliyopo katika mpango wake wa miaka mitano kwa lengo la kuinua hali za maisha ya wananchi wa Tunduru Kusini,kuleta maendeleo ya kiuchumi katika wilaya ya Tunduru pamoja na kuchochea uwajibikaji wa jamii kwenye mambo mbalimbali ikiwemo Afya,Elimu na maji.

“nilitamani sana katika kipindi changu cha miaka mitano kuwasomesha watoto 4000 wa shule za msingi na sekondari ambao nilifanikiwa kuwanunulia sale na mahitaji yote ya shule,lakini nasikitika sana kusema baadhi ya wazazi wameniangusha kwani kuna watoto ambao  wameacha shule bila sababu ya msingi”alisema.

Amewataka wazazi wilayani Tunduru, kuhakikisha wanapeleka  watoto wao  shule kupata elimu, badala ya kuwarithisha kazi za nyumbani ikiwemo mashamba ya korosho  kwani elimu  ndiyo  itakayomaliza tatizo la umaskini  na ujinga kwenye familia zao.

Sambamba na hilo, Mpakate amewataka wananchi wa  Jimbo la Tunduru Kusini kuepuka  vitendo vya kuhujumu miradi ya maendeleo inayoendelea kutekelezwa  katika maeneo yao,badala yake waone fahari kutunza na kulinda ili iweze kuleta tija na kurahisishia  shughuli za maendeleo na hivyo kuondokana na umaskini.

Diwani wa kata ya Chiwana Rashid Makunganya amemshukuru Mbunge huyo kwa kutoa shilingi milioni 12 ambazo zimekwenda kutatua kero ya upungufu wa vyumba  vya madarasa na  matundu ya vyoo  katika  shule za msingi  Chiwana.

Makunganya amewataka watendaji wa vijiji na kata, kuhakikisha fedha hizo zinatumika  vizuri  badala ya kuzielekeza mifukoni mwao jambo linaloweza kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria.

Alisema, Jimbo la Tunduru kusini limepata Mbunge mpenda maendeleo,kwa hiyo amewataka wananchi kuendelea kuunga mkono juhudi zake ili  kwa pamoja waweze kumaliza kero zilizopo  badala ya jukumu hilo kumuachia Mbunge pekee yake.

Hata hivyo, baadhi ya wananchi wa kijiji hicho wakiongozwa na  Said Sandali wameiomba Serikali kuongeza idadi ya watumishi katika zahanati ya Chiwana kwani waliopo hawatoshi  jambo linalosababisha kuzorota kwa baadhi ya huduma katika zahanati hiyo pindi mmoja wapo anapopata dharura ya kuwa nje ya kituo chake cha kazi.