Home Mchanganyiko HALMASHAURI YA MJI KONDOA  KUTOA CHANJO ZOTE KWA MIFUGO

HALMASHAURI YA MJI KONDOA  KUTOA CHANJO ZOTE KWA MIFUGO

0

Afisa Mifugo na Uvuvi Halmashauri ya Mji Kondoa Bi. Monica Kimario akivuta dawa tayari kwa kuanza zoezi la utoaji wa chanjo kata ya Kingale

……………………………………………………………………………………………………………..

Idara ya Mifugo na Uvuvi Halmashauri ya Mji Kondoa imejipanga kuendelea kutoa chanjo ya magonjwa ya Mifugo kulingana na kalenda ya chanjo inavyoonyesha kwa mwaka mzima.

Hayo yalibainishwa na Afisa Mifugo na Uvuvi wa Halmashauri ya Mji Bi. Monica Kimario wakati wa utoaji wa chanjo ya ugonjwa wa Kimeta na Chambavu kwa mifugo ya kata ya Kingale.

“Nawasihi sana wafugaji wa Kata ya Kingale washiriki katika zoezi hili kwa kuleta mifugo yao katika maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya utoaji wa chanjo ili kudhibiti magonjwa yatakayotokea bila kufanya hivyo mifugo itashambuliwa na magonjwa hayo,”alisema Bi. Monica

Aidha aliwashauri wafugaji kuleta mifugo yao yote waliyonayo ili kupata chanjo kwani baadhi ya wafugaji huleta mifugo michache kupata chanjo na kuficha mingine hali inayohatarisha kutokea kwa magonjwa kwa mifugo ambayo haitapata chanjo.

“Chanjo hii ni salama kabisa na inatolewa na wataalam wa mifugo na hakuna matatizo yoyote yaliyotolewa kwa maeneo ambayo chanjo imetolewa na nawahisi wafugaji kutumia wataalam wa mifugo katika matibabu ya mifugo yao ili kuepukana na kupewa chanjo isiyo sahihi na hatari kwa mifugo yao,”alisisitiza Bi. Monica.

Hata hivyo alitaja faida za mifugo kupatiwa chanjo kuwa ni pamoja na kudhibiti magonjwa, kuongeza uwezo wa wanyama kujikinga na maradhi, kupunguza gharama za matibabu na kuzuia magonjwa ya kuambukiza kutoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu.

“Hasara za kutopata chanjo nazo zipo ambazo ni kupoteza mifugo kwa vifo, kupunguza uzalishaji wa mifugo na uambukizaji wa magonjwa ya mifugo kutoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu,”alibainisha Bi. Monica.

Halmashauri ya Mji Kondoa imejipanga kuhakikisha wanapunguza vifo vya mifugo na kuongeza uzalishaji kwa kutoa chanjo ambapo kwasasa imeanza kutolewa katika kata ya Kingale kwa magonjwa ya Kimeta na Chambavu ambapo kwa Halmashauri yote jumla ya ng’ombe 26,696, mbuzi 18,417 na kondoo 2782 wanatarajia kuchomwa chanjo hiyo.