Mkuu wa Kitengo cha TEHAMA Idara ya Uhamiaji Kamishna Msaidizi Mwandamizi Mohammed Bakar (kati kati) na Mdhibiti wa Pasipoti Kamishna Msaidizi Dorah Luoga (kulia) wakiwa pamoja na Mkurugenzi wa Airtel Money Isaack Nchunda wakionyesha bango baada ya pamoja kusaidia ushirikiano ambapo kwa sasa Watanzania wataweza kulipia pasipoti kwa kutumia Airtel Money.
Mkuu wa Kitengo cha TEHAMA Idara ya Uhamiaji Kamishna Msaidizi Mwandamizi Mohammed Bakar akizungumza wakati wa kuzindua ushirikiano baina ya Idara ya Uhamiaji na Airtel ambapo kwa sasa Watanzania wataweza kulipia pasipoti kwa kutumia Airtel Money. Kulia ni kuu wa Kitengo cha TEHAMA Idara ya Uhamiaji Kamishna Msaidizi Mwandamizi Mohammed Bakar.
*******************************
Dar es Salaam Alhamisi 5 Machi 2020….Kampuni ya simu za mkononi ya Airtel Tanzania kwa kushirikiana na Idara ya Uhamiaji nchini leo wametangaza kuzindua rasmi huduma ya kulipia gharama za pasi za kusafiria kwa kupitia huduma za “Airtel Money”. Uzinduzi huo wa malipo ya ada za pasi za kusafiria kwa njia ya “Airtel Money” ni muendelezo wa ushirikiano uliopo kati ya Kampuni ya Airtel na Serikali katika kutumia mfumo wa kisasa wa kiteknolojia kufanya malipo ya huduma na bidhaa mbali mbali njia ambayo ni salama, haraka na nafuu.
Akizungumza leo jijini Dar es Salaam wakati wa kutangaza huduma hiyo ya kulipia huduma za Pasi za kusafiria kwa kutumia huduma ya Airtel Money, Mkuu wa Kitengo cha TEHAMA Idara ya Uhamiaji, Kamishna Msaidizi Mohamed Bakar alisema kuwa, hiyo ni moja ya njia rahisi ambayo itawafanya Watanzania kulipia gharama za ada za pasi za kusafiria kwa urahisi zaidi na popote walipo.
‘Kama mnavyojua, fomu za maombi ya Pasipoti zinajazwa kwa njia ya mtandao. Hii imekuwa ni njia rahisi sana kwani Mtanzania popote alipo haitaji kutembelea ofisi za Uhamiaji ili kupata fomu ya Pasipoti, bali anaweza kutembelea tovuti ya Idara ya Uhamiaji,. akajaza fomu yake na kuilipia kwa njia ya mtandao na kisha kuiwasilisha fomu hiyo Ofisi ya Uhamiaji kwa taratibu zinazofuata.
Kwa sababu hiyo, leo ni siku nyingine muhimu kwetu kuweza kuungana na wenzetu wa Airtel ili kurahishisha malipo ya ada za pasi za kusafiria,’ alisema Kamishna Bakar.
Serikali ilishaweka mikakati ya kutumia njia ya kisasa katika kufanya malipo ya huduma mbalimbali kwa haraka na usalama na kuzielekeza taasisi zake zote kutumia Mfumo wa Serikali wa malipo kwa njia ya Mtandao GePG. Mfumo huu umerahishisha sana malipo na umekuja na faida nyingi kama vile kurahisisha malipo, kuimarisha utunzaji wa kumbukumbu, kupunguza upotevu wa mapato ya Serikali, kuondoa mianya ya rushwa pamoja na kuongeza mapato ya serikali. Kwa sababu hiyo, nachukua fursa hii kuwapongeza Airtel kwa kuweza kuungana nasi ili kuwawezesha Watanzania kufanya malipo ya pasi za kusafiria kwa kutumia Airtel Money. Natoa wito kwa watanzania kutumia huduma hii ambayo kufanya malipo yao kwani ni salama na rahisi kutumia, Kamishina Bakar aliongeza.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Airtel Money Tanzania Isack Nchunda alisema, ‘Kuunga mkono juhudi za Serikali imekuwa ni moja ya agenda kubwa kwetu. Tunaelewa umuhimu wa Serikali wa kuhakikisha kuwa malipo yote ya kwenda serikalini yanafanyika kwa mfumo wa GePG. Tutaendelea kushirikiana na taasisi pamoja na mashirika mengine ya serikali kwa ajili ya kutoa suluhisho ili kutimiza haya’.
Nchunda alitoa wito kwa Watanzania kuendelea kutumia huduma za kielectroniki za Airtel kwani zina ubunifu mkubwa pamoja na kuwa rafiki. “Ni muhimu kwa Watanzania kuelewa kuwa Airtel inamilikiwa na Watanzania kupitia serikali kwa asilimia 49. Na hii inamaanisha kuwa ukitumia huduma za Airtel unatumia kilicho cha kwetu. Nia yetu ni kuendelea kutoa huduma ambazo zinakidhi matakwa ya sasa ya kidigitali.
Nchunda aliongeza kuwa ili wateja waweze kukamilisha malipo ya huduma za pasi za kusafiria wafuate njia ifuatayo:
Piga namba ya Airtel Money *150*60# na chagua malipo ya Serikali-Namba 5
Weka namba ya kumbukumbu (ziko namba 12)
Weka kiasi cha malipo
Weka namba ya siri kuruhusu malipo
Mara baada ya kukamilisha muamuala, mteja atapokea ujumbe mfupi wa maneno kuthibitisha malipo yake. Risiti hiyo ya kielectroniki itakuwa ndio uthibitisho wa malipo na ni rahisi kwa kuhifadhi au kwa kufuatilia kwa baadae kwani haiwezi kupotea au kuharibika.
Airtel Money kwa sasa imeunganisha kwa kulipia huduma za malipo zaidi ya 1,000 kwa watoa huduma na vile vile mabenki pamoja na taasisi za kifedha zaidi ya 40 ambapo mteja anaweza kuweka au kutoa pesa zake akiwa popote. Airtel Money pia inazidi kukua ambapo kwa sasa ina maduka ya Airtel Money na matawi zaidi ya 1500 yanayotoa huduma mbalimbali pamoja na bidhaa za Airtel.