Mratibu wa vijana Wizara ya Kilimo Revelian Ngaiza akizungumza wakati wa ufunguzi wa kongamano la vijana wanaoshiriki shughuli za kilimo,mifugo na uvuvi toka mikoa ya Tabora,Singida,Dodoma na Kigoma
Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri )aliyevaa tai katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na vijana wanaoshiriki kongamano la fursa za kilimo,mifugo na uvuvi mjini Tabora leo
Sehemu ya viongozi na washiriki wakifuatilia mada kuhusu fursa za kilimo ,mifugo na uvuvi kwenye kongamano mjini Tabora leo.
……………………………………………………………………………………………….
Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri amewataka vijana kutumia fursa ya uwepo wa miundombinu iliyoboreshwa na serikali kukuza tija ya uzalishaji mazao ya kilimo na mifugo
Ametoa kauli hiyo leo (04.03.2020) wakati akifungua kongamano la vijana katika kilimo linaloshirikisha vijana wapatao 340 toka mikoa ya Tabora, Singida ,Kigoma na Dodoma kwenye ukumbi wa Mtemi Isike Mwanakiyungi mjini Tabora.
“Mkoa wa Tabora ni wa tatu kwa ukubwa nchini ukiwa na kilometa za mraba 75,000 zinazofaa kwa kilimo na ufugaji “ alisema Mkuu wa Mkoa Mwanri na kuongeza kuwa Tabora ina watu milioni 2.7 wenye nguvu za kufanya kazi.
Mwanri amewaeleza vijana hao kuwa Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Dkt John Pombe Magufu imefanikiwa kukamilisha miradi mingi ya miundombinu kama barabara na reli hivyo kufanya mazingira ya ufanyaji kazi za kilimo na mifugo kuwa mazuri.
“ KIjana fikiri tofauti,fikiri kwa usahihi na fikiri kwa kuangalia mbele kuwa baada ya kongamano hili utakuwa vipi kiuchumi” alisisitiza Mwanri
Mkuu wa mkoa huyo alitaja fursa ya uwepo ng’ombe milioni 2.7 ikitumiwa vizuri na itasaidia kukuza ajira kama uuzaji ,usambazaji wa ngozi na uchakataji wake.
Fursa nyingine kwa vijana ni uwepo wa zao la tumbaku kwa takwimu zinaonyesha asilimia 60 ya tumbaku yote nchini inatoka Tabora pia vijana wana uwezo wa kuzalisha mpunga unaostawi kwenye wilaya zote za Tabora.
Aliongeza kusema vijana wa mikoa ya kanda ya kati wanaweza sasa kufikisha mazao yao kwenye masoko hususani makao makuu ya nchi,Dodoma kutokana na urahisi wa kusafirisha kawa njia ya barabara na reli.
“Vijana nendeni mkauze mchele badala ya mpunga,unga badala ya mahindi kwa kuwa umeme upo wa uhakika hadi ngazi ya vijiji.Fungueni viwanda vidogo vya kuchakata mazao” alisema Mwanri
Katika kuhakikisha vijana wanakuwa na mitaji ya uhakika ,Mwanri amewaonya vijana kuacha kwenda kukopa fedha benki au Halmashauri bila ya kuwa na kazi ya kufanya.
Aliwasihi vijana wajiunge katika ushirika kwani ndio njia pekee ya na rahisi ya serikali kuwafikia na kuwasaidia wanyonge kujikwamua kiuchumi.
“Vijana fikirini tofauti ili muweze kusonga mbele,acheni tabia ya kulalamika kukosa fursa,kilimo kinalipa” alisema Mwanri na kuwa ‘’fursa hhazitolewi bali zinzchukuliwa
Kwa upande wake Mwakilishi wa mwakilishi Mkazi wa Shirika la Chakula na Kilimo la umoja wa Mataifa (FAO) nchini Stella Kimambo ameipongeza serikali ya Tanzania kwa hatua zake za kutekeleza mkakati wa vijana kwenye kilimo kwani umesaidia kuongeza ajira
Alisema FAO wanaamini kuwa vijana wakijiunga kwenye shughuli za kilimo ,uchumi wa nchi na kaya utaimarika zaidi.
Akizungumza kwenye kongamano hilo Mratibu wa Vijana, Wizara ya Kilimo Revelian Ngaiza alisema wizara inatekeleza mkakati wa vijana wa miaka mitano katika kilimo ili kuwezesha watambue aina ya fursa zilizopo ili kuzalisha ajira na kukuza uchumi.
Ngiza alisema hadi sasa tayari makongamano mawili kwenye kanda za Songwe na Njombe yamefanyika na vijana wameonyesha shauku kubwa kushiriki kwenye maeneo hayo.
“ Tumepanga kufanya makongamano kwenye mikoa yote ya Tanzania bara ili kuwafikishia elimu,uzoefu na nanma ya kutumia rasilimali ardhi kuwa fursa ya vijana kujiajili na kuajili wengine” alisema Ngaiza.
Kongamano hilo la siku mbili linafanyika sambamba na lingine mkoani Arusha kwa uratibu wa Wizara ya Kilimo na wadau wa kilimo,mifugo na uvuvi toka sekta binasfi na za umma.