Waziri Mkuu mstaafu Mizengo Pinda (katikati) akiwa na Katibu Mkuu wa Bakwata Mkoa wa Singida, Sheikh.Alhajj Burhan Mlau (kulia) na (wa kwanza kushoto ni Sheikh wa Shiha mkoani Arusha, Abubakari Hussein Sombi.
Waziri Mkuu mstaafu Mizengo Pinda (katikati) akiwa na baadhi ya viongozi wa dini ya Kiislamu kwenye harambee hiyo.
Waziri Mkuu mstaafu Mizengo Pinda (katikati) akiwa na baadhi ya viongozi wa dini ya Kiislamu kwenye harambee hiyo.
Tukio la harambee likiendelea.
Na Godwin Myovela, Singida
WAZIRI Mkuu mstaafu Mizengo Pinda, juzi ameongoza waislamu katika harambee ya kuchangia ujenzi wa ofisi ya Baraza la Kuu la Waislamu nchini (BAKWATA) inayotarajiwa kujengwa eneo la Ilongero, Wilaya ya Singida Vijijini , mkoani hapa.
Zaidi ya shilingi milioni 40 zimepatikana katika vipindi viwili tofauti vya zoezi la harambee hiyo, ambapo awamu ya kwanza Pinda aliwakilishwa na Katibu wa Bakwata Mkoa wa Singida, Sheikh Alhajj Burhan Mlau ambapo jumla ya shilingi milioni 3.6, sambamba na mifuko 198 ya saruji vilipatikana.
Awamu ya pili ya harambee hiyo ilifanyika mwishoni mwa wiki ikiongozwa na Pinda mwenyewe, ambapo jumla ya shilingi milioni 37 sambamba na mifuko 44 ya saruji vilipatikana na kufanya harambee hiyo kuvuka nusu ya malengo yake. Jumla ya fedha yote inayohitajika hadi kukamilisha ujenzi huo ni shilingi milioni 65.5.
Akizungumza na waandishi wa habari mkoani hapa jana, Mlau alimpongeza Waziri Mkuu mstaafu Pinda na serikali ya mkoa kwa namna wanavyojitoa kikamilifu katika kusaidia shughuli mbalimbali za dini ya kiislamu kwenye mkoa huo, na hasa pale muda wote wanapohitajika kufanya hivyo.
“Tunamshukuru sana Pinda kwa kutujali na kututhamini, kwakweli michango yote hii imefanyika kwa hamasa yake na ametuunga mkono kwa nguvu zote,” alisema.
Aidha, Mlau alimpongeza Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dkt Rehema Nchimbi ambaye mara kwa mara hupendelea kumuita “Hajjat” (Mavazi yake siku zote ni mithili ya mwanamke aliyekwenda hijja) kwa kuwa karibu na dini hiyo ya Kiislamu na kujitoa kila mara anapohitajika.
“Niwasihi waislamu wenzangu tuwe waaminifu na tutumie michango hii kwa malengo tarajiwa, na pia tunakaribisha wengine wote ambao wangependa kutuunga mkono ili hatimaye tuweze kufanikisha ujenzi huu muhimu,” alisema Alhajj Mlau.
Ujenzi wa ofisi hiyo unatarajiwa kuanza mwishoni mwa mwezi Machi mwaka huu, baada ya taratibu za maandalizi yake kukamilika.