…………………………………………………………………………………………….
*Ni baada ya kushindwa kukagua madaraja kwenye eneo lake
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameagiza Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROAD), mkoa wa Morogoro, Mhandisi Godwin Andalwisye arejeshwe wizarani na nafasi yake ijazwe na mtu mwingine mara moja baada ya kuzembea kutimiza wajibu wake.
Pia, Waziri Mkuu ametoa onyo kwa Mameneja wa TANROAD wa mikoa yote nchini waache kukaa maofisini na badala yake wahakikishe wanatekeleza majukumu yao ipasavyo ikiwa ni pamoja na kufanya ukaguzi wa mara kwa mara wa madaraja yote ili kujiridhisha na hali ya usalama hususani katika kipindi hiki cha mvua.
Uamuzi huo umekuja baada ya kiongozi huyo kushindwa kufanya ukaguzi wa usala wa madaraja yaliyoko kwenye mkoa wake na kubaini kama kuna daraja linamatatizo hali iliyosababisha daraja la Kiyegeya lililopo wilayani Kilosa ambalo linaunganisha mkoa wa Morogoro na Dodoma kuvunjika.
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo(Jumatano, Machi 4, 2020) baada ya kutembelea eneo hilo na kukagua ukarabati ili kurejesha mawasiliano ya barabara. Waziri Mkuu ameshuhudia mrundikano wa magari na abiria hali ambayo haikumfurahisha.
“Hivi unajua udhahifu wako ni kwa sababu hukufanya ukaguzi kuona kama daraja limejaa mchanga au uchafu ambao umesababisha kipenyo cha kupitisha maji kuwa kidogo na maji yakalazimika kupanda juu hali ambayo ilisababisha daraja hili kusombwa na maji.”
Amesema wakati njia hiyo inarekebishwa itengenezwe njia nyingine ya muda ili kuweza kupitisha magari na kisha Serikali itachukua hatua baada ya kubaini nini kimesababisha.
Ili kuharakisha kazi hiyo inakamilika kwa haraka, Waziri Mkuu ameagiza Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Mhandisi Isack Kamwelwe, Katibu Mkuu wa wizara hiyo pamoja na wahandisi wote wa TANROAD mkoa wa Morogoro na Dodoma leo wakutane kwenye eneo la tukio na wahakikishe kuanzia kesho (Alhamisi, Machi 5, 2020) njia hiyo iwe imefunguka.
Kadhalika, Waziri Mkuu amesema atawasiliana na Mkuu wa Majeshi, Generali Venance Mabeyo ili aweze kupata msaada wa wanajeshi ili waongeze nguvu katika kuhakikisha kwamba mawasialaino yanarejea kwa haraka.
Akiwapa pole madereva na watumiaji wengine wa barabara waliokwama katika eneo hilo, Waziri Mkuu amesema “Nimetumwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli kuja kuwapa pole na kuwahakikisha kwamba Serikali inafanya kila linalowezekana ili kuifungua barabara hii.”