Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni katikati Mhe. Benjamini Sitta akiwa na Naibu Meya George Manyama na Kaimu Mkurugenzi Dk. Patricia Henjewele wakiwa katka kikao cha robo ya pili cha baraza la madiwani.
Mbunge wa jimbo la Kinondoni, Mhe. Maulid Mtulia akizungumza wakati wa kikao cha robo ya pili cha Baraza la Madiwani kilichofanyika katika ukumbi wa Manispaa.
Mchumi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, Nasoro Shemzigwa akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika baraza la madiwani lililofanyika katika ukumbi wa manispaa hiyo.
****************************
Baraza la madiwani Manispaa ya Kinondoni limepongeza wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (TARURA) kwa usimamizi na ukaratabati mzuri wa barabara zilizopo katika Halmashauri hiyo.
Pongezi hizo zimetolewa katika kikao cha kawaida cha robo ya pili cha baraza la madiwani ambapo madiwani hao wameeleza kuwa TARURA imefanya kazi kubwa ya kutengeneza barabara katika maeneo mbalimbali ndani ya Halmashauri hiyo na hivyo kuwezesha mitaa mbalimbali kuwa na muonekano mzuri.
Awali Meneja wa TARURA wa Halmashauri hiyo, Mhandisi Leopold Runji alisema kuwa mtandao wa barabara katika Manispaa hiyo ni kilomita 1700 ambapo hadi sasa Km. 170 zimejengwa kwa kiwango cha lami, Km. 390 zimejengwa kwa kiwango cha changarawe (Moram) huku Km. 1140 katika kiwango cha vumbi kwa kusawazishwa na Greda.
Mhandisi Runji alifafanua kuwa mkakati wa TARURA kwa barabara za vumbi ambazo hazijafikiwa na huduma ya ukarabati kwa maeneo ya Kata na Mitaa mbalimbali zimewekwa kwenye bajeti ya mwaka 2020/2021 ambapo zaidi ya Km. 197 zitafanyiwa ukarabati huo.
Katika hatua nyingine Baraza hizo limepitisha taarifa mbalimbali za kamati za kudumu za Halmashauri hiyo zilizowasilishwa na wenyeviti ambapo kamati hizo ni Uchumi, Afya na Elimu, Kamati ya Mipango miji ujenzi na mazingira, Kamati ya Maadili, Kamati ya Ukimwi pamoja na Kamati ya fedha na uongozi.
Awali akisoma Taarifa ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa kipindi cha robo ya pili ya mwaka , Kaimu Mkurugenzi Dk. Patricia Henjewele alisema kuwa katika kipindi cha mwaka wa fedha wa 2019/2020, Halmashauri ilikisia kukusanya na kupokea kiasi cha sh. Bil.150.6 ambapo kati ya fedha hizo Tsh. Bil. 110.5 ni ruzuku kutoka Serikali kuu na Tsh. Bil. 40. ni fedha za makusanyo ya ndani.
Kuhusu miradi ya maendeleo, Dk. Henjewele alieleza kuwa katika mwaka wa fedha wa 2019/2020, Halmashauri hiyo ilikisia kutumia kiasi cha Tsh. Bil.81.5 kwa ajili ya kugharamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo kutokana na vyanzo mbalimbali vya mapato pamoja na nguvu za jamii.
Alivitaja vyanzo hivyo vya fedha kuwa ni Tsh. Bil. 19.8 zinatokana na mapato ya ndani na kiasi cha Tsh. Bil. 61. 5 ni ruzuku kutoka Serikali kuu.